NEWS

Saturday 9 December 2023

Mkurugenzi wa HSF aja na harambee ya kuchangia ujenzi wa wodi ya mama na mtoto Kituo cha Afya Sungusungu



Mkurugenzi Mwanzilishi wa Shirika la HSF, Emmyliana Range.
-------------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Nyamongo
-----------------------------------------------------

Shirika la Health and Safe Delivery Foundation (HSF) linaandaa harambee kubwa itakayowaleta pamoja wadau wa maendeleo kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa jengo la wodi ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya Nyangoto - kinachojulikana pia kwa jina la Sungusungu kilichopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara. 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mwanzilishi wa HSF, Emmyliana Range, harambee hiyo itafanyika Desemba 15, 2023 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ingwe mjini Nyamongo, kilomita chache kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara. 

“Lengo la harambee hiyo ni kupata shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kugharimia ujenzi wa jengo la ghorofa moja la wodi ya mama na mtoto,” alisema Emmyliana katika mazungumzo na Gazeti la Sauti ya Mara mjini hapa juzi. 

Alibainisha kuwa wadau zaidi ya 200 wakiwemo wachimbaji wa madini, wakandarasi wanaofanya kazi na mgodi wa Barrick North Mara, na sekta ya afya wamealikwa kushiriki harambee hiyo. 

Alisema ufinyu wa wodi ya mama na mtoto, na msongamano wa wanawakwe wanaokwenda kujifungua katika Kituo cha Afya Nyangoto, ndio umemsukuma kuandaa harambee hiyo, ili kuboresha huduma kwa kundi hilo la jamii. 

“Mimi kama mzawa wa Nyamongo, natamani kila mama anayejifungua katika Kituo cha Afya Sungusungu apate huduma nzuri kama ambavyo mimi nilipata wakati wa kujifungua katika hospitali za AMI na Agakhan jijini Dar es Salaam,” alisema Emmyliana. 

Hivyo Mkurugenzi Mwanzilishi huyo wa HSF alitoa wito wa kuhamasisha wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Nyamongo kujitokeza kwa wingi, ili kufanikisha harambee hiyo - inayolenga kuboresha huduma ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya Nyangoto. 
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages