NEWS

Tuesday 5 December 2023

MVIWANYA waahidi neema kwa wakulima, wafugaji Tarime Vijijini



Mratibu wa MVIWANYA, Joel Nguvava (katikati) katika picha ya pamoja na wanachama wa vikundi vya wakulima na wafugaji mara baada ya kikao chao kilichofanyika kata ya Nyakonga wilayani Tarime, jana Jumanne. (Picha na Godfrey Marwa)
-------------------------------------------------------

Na Godfrey Marwa
wa Mara Online, Tarime
-------------------------------------


Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Nyancha (MVIWANYA) umeahidi kupeleka mafunzo ya ujasiriamali na kilimo kwa vikundi vitano vya wakulima na wafugaji vilivyo chini ya mtandao huo katika kata ya Nyakonga wilayani Tarime, Mara.

Mratibu wa MVIWANYA, Joel Nguvava alitoa ahadi hiyo kwenye kikao cha vikundi hivyo (Sky Group, Upendo, Yerusalemu, Mkombozi na Tumaini), kilichofanyika katani humo jana Jumanne.

“Tutatoa fursa ya kujifunza cherehani (ushonaji), useremala na kompyuta. Tunaendelea kuongea na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) kupata sehemu kwa ajili ya kujifunzia. Tutatoa pia mafunzo ya kilimo cha bustani za mboga mboga na mbegu, na madawa tutawapa bure,” alisema Nguvava.


Nguvava akisisitiza jambo katika kikao hicho

Katika hotuba yake, Mwenyekiti wa MVIWANYA Tanzania, Oyoo Mande aliwahimiza wanachama wa vikundi hivyo, hususan vijana kuchangamkia fursa za kilimo chenye tija zinazojitokeza kwao.

“Vijana msione kilimo kama adhabu, elimu ya kilimo mesto ni muhimu ipelekwe kila kona vijijini ili kuleta mabadiliko chanya kwa wakulima. Shirikianeni na MVIWANYA na wadau walio tayari kusaidia wakulima na wafugaji,” alisema Mande.


Oyoo Mande

Mwanachama wa Sky Group, Mussa Shaban alishukuru MVIWANYA na kuuomba mtandao huo kuendeleza mpango wa kuwapatia wakulima elimu ya kilimo mseto.

“Tunaomba elimu ya kilimo mseto iwe endelevu, na wajasiriamali wapatiwe elimu ya kutumia fedha za mikopo kutoka kwenye vikundi na taasisi za kifedha,” alisema mkulima huyo na kuendelea:

“Bei ya mbolea ipunguzwe na maghala ya mbolea yasogezwe vijijini ili kupunguza gharama ya kwenda kuitafuta mjini - kama kweli Serikali ina nia ya dhati ya kutekeleza kwa vitendo sera ya kilimo mesto.”


Mussa Shaban

MVIWANYA wanatekeleza shughuli zake kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Vi Agroforestry ambalo linahamasisha kutetea na kuwezesha kaulimbiu ya kilimo mseto kwa vitendo, ikiwa ni Pamoja na kusaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages