NEWS

Tuesday 12 December 2023

Mwenyekiti CCM Mara awatwisha mizigo Waziri Slaa, Naibu Waziri MahundiMwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa.
--------------------------------------------------

NA MWANDISHI
WETU, Musoma
-------------------------


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kimependekeza mradi wa maji wa Ziwa Victoria upanuliwe ili uweze kuwafikia wananchi wa Nyamongo na Serengeti mkoani Mara.

Sambamba na hilo, chama hicho tawala pia kimezitaka Wizara za Ardhi na Fedha kuharakisha ulipaji wa fidia wa wananchi wa wanaohamishwa kupisha eneo la Nyatwali wilayani Bunda.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, aliwasilisha maelekezo hayo kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Slaa na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, walipomtembelea ofisini kwake mjini Musoma juzi, wakiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani humo.


Kutoka kulia mwenye shati la kijani ni Mwenyekiti Chandi, Waziri Slaa na Naibu Waziri Mahundi wakati wa mahojiano na waandishi wa habari mjini Musoma, jana.
----------------------------------------------------

Chandi alimwomba Waziri Slaa kumfikishia Waziri wa Fedha, Dkt Mwigulu Nchemba ujumbe huo wa kulipa fidia za wananchi wanaohamishwa Nyatwali haraka iwezekanavyo.

“Uthamini ulishafanyika na sasa ni zaidi ya miaka miwili wananchi hawafanyi chochote pale [Nyatwali],” Chandi alimwambia Waziri huyo mwenye dhamana ya masuala ya ardhi nchini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mahundi alisema amepokea ombi la Chandi la kuufikisha mradi wa maji wa Ziwa Victoria Nyamongo na Serengeti. “Suala hilo litaingizwa kwenye mpango,” aliahidi bila kufafanua zaidi.

Mradi wa maji wa Ziwa Victria ambao umeshaanza kutekelezwa, unatarajiwa kunufaisha maelfu ya wananchi wa wilaya za Tarime na Rorya katika mkoa wa Mara ambao unapakana na ziwa hilo.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages