NEWS

Tuesday 12 December 2023

Wanawake wajasiriamali 34 wahitimu mafunzo ya programu ya AWE Mara, Serikali yapongeza Ubalozi wa MarekaniWaliokaa ni RC Yahaya Nawanda (katikati), Mwakilishi wa Ubalozi wa Marekani, Jeanne Clark (wa tatu kulia), Gachuma (wa pili kulia), DC Tarime, Kanali Michael Mntenjele na viongozi wengine katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo ya AWE mkoani Mara, jana. (Picha na Sauti ya Mara)
----------------------------------------------------

NA MWANDISHI
WETU, Tarime
-----------------------------


WANAWAKE 34 wamehitimu mafunzo ya kuwajengea ujuzi na mbinu za kujiendeleza kiuchumi, chini ya programu ya Chuo cha Wanawake Wajasiriamali (AWE) inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Ubalozi wake nchini Tanzania.

Mahafali ya wahitimu hao yalifanyika jana katika Hoteli ya CMG mjini Tarime, na kuhudhuriwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Dkt Yahaya Nawanda, Mwenyekiti wa Kundi la Kampuni za CMG na Mbia wa AWE mkoani Mara, Christopher Gachuma na Afisa wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania anayeshughulikia masuala ya umma, Jeanne Clark.

Katika hotuba yake, RC Nawanda ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliupongeza Ubalozi wa Marekani, na kuwataka wahitimu hao kutumia ujuzi walioupata kujiendeleza kibiashra na kutimiza ndoto zao, lakini pia kufikisha elimu hiyo kwa wanawake wengine ambao hawakupata bahati hiyo.


Mhitimu akikabidhiwa cheti.

“Tumieni elimu hii kubadilisha biashara zenu na fikira zenu na kusaidia wanawake wengine na muwe mabalozi wazuri,” Dkt Nawanda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa jirani wa Simiyu, aliwambia wahitimu hao.

Alitumia nafasi hiyo pia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kujenga mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo nchini.

Kwa upande wake, Clark alimpongeza Gachuma kwa kusaidia kufanikisha mafunzo hayo kufanyikika mkoani Mara, na kuahidi kuwa Ubalozi wa Marekani utaendelea kusaidia wahitumu hao.


Clark (kushoto) akizungumza.

Naye Gachuma ambaye ni mfanyabiashara maarufu Kanda ya Ziwa, aliushukuru Ubalozi wa Marekani kwa kukubali ombi lake la kuleta mafunzo hayo mkoani Mara.

Hata hivyo, Gachuma alisema mafanikio ya wahitimu hao yatachagizwa na dhana ya kujituma kufanya kazi kwa bidii, umakini na weledi.


Gachuma akizungumza.

Awali, Mratibu wa AWE Tanzania, Dkt Victoria Kisyombe alisema programu hiyo ilianzishwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani mwaka 2019, na kwamba hadi sasa inatekelezwa katika nchi 20 duniani ikiwemo Tanzania.

“Programu hii ya AWE inachangia kwa kiasi kikubwa jitihada za Serikali yetu [ya Tanzania] za kuwaendeleza wanawake kiuchumi na kielimu,” alisema.


Dkt Kisyombe (kushoto) akizungumza.

Kwa mujibu wa Dkt Kisyombe, hadi sasa programu hiyo imewezesha wanawake wajasiriamali 350 kupata mafunzo katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Pwani, Kigoma, Kagera, Visiwa vya Zanzibar (Unguja na Pemba) na Mara.

Katika mahafali hayo ya wahitimu wa mafunzo ya AWE, RC Nawanda pia alipata fursa ya kukagua mabanda ya bidhaa mbalimbali za wahitimu hao na kujionea ubunifu wa kazi walizoanzisha kwa ajili ya kujipatia kipato.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages