NEWS

Monday, 18 December 2023

Nyangwine achangisha shilingi zaidi ya milioni 200 katika harambee ya ujenzi wa jengo la Kanisa Katoliki Nyamwaga



Askofu Michael Msonganzila akifurahi kupokea hundi yenye thamani ya shilingi milioni 20 kutoka kwa mdau wa maendeleo Nyambari Nyangwine aliyeongoza harambee ya ujenzi wa jengo la Kanisa Katoliki Parokia ya Nyamwaga na kufanikisha upatikanaji wa shilingi zaidi ya milioni 200 kanisani hapo jana Juamapili. Kushoto ni mdau mwingine wa maendeleo Anitha Waitara. (Picha na Godfrey Marwa)
-------------------------------------------------------

NA CHRISTOPHER GAMAINA
---------------------------------------------


MDAU wa maendeleo, Nyambari Nyangwine, ameongoza harambee iliyofanikisha upatikanaji wa shilingi zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya kuchangia gharama za ujenzi wa jengo jipya la Kanisa Katoliki Parokia ya Nyamwaga, wilayani Tarime.

Harambee hiyo ilifanyika jana Jumapili kwenye viwanja vya kanisa hilo kijijini Keisangora, ambapo pia ilihudhuriwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila na Paroko wa Parokia ya Nyamwaga, Padre Julius Manyonyi.

Katika harambee hiyo, Nyangwine ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Tarime kwa tiketi ya chama tawala - CCM, alisindikizwa na rafiki zake kutoka Dar es Salaam, Mwanza, watumishi wa kiroho na wakazi wa Tarime, huku yeye peke yake akichangia shilingi milioni 20 taslimu.


Askofu Msonganzila akisalimiana na kumpokea Nyangwine (wa pili kulia) kanisani hapo.

Katika hotuba yake, Nyangwine aliwashukuru watu wote waliomuunga mkono katika kufanikisha harambee hiyo, akisema michango yao itakumbukwa na kuthaminiwa daima.

“Nimefurahi sana, mimi ni Msabato lakini wote tunajenga nyumba moja na kumtumainia Mungu mmoja. Ninaomba umoja, amani, upendo na ushirikiano vidumu katika mioyo yetu,” alisema Nyangwine ambaye ni Mwenyekiti wa Nyambari Nyangwine Group of Companies Ltd (NNGCL).

Alitumia nafasi hiyo pia kupendekeza wazo kwa wazaliwa wa Tarime wanaoishi katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam na Mwanza kuanzisha mfuko wa kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo.

Naye Askofu Msonganzila mbali na kumshukuru Nyangwine na wachangiaji wote wa harambee hiyo, aliitaka jamii kudumisha amani, maadili na moyo wa kuchangia maendeleo.

Kwa upande wake, Askafu Msonganzila alichangia shilingi milioni mbili taslimu katika harambee hiyo na kuahidi mchango wa matofali 100.

Miongoni mwa wachangiaji wengine, ni Anitha Gimero Waitara ambaye alimuunga mkono Nyangwine kwa kuchangia shilingi milioni 14 katika harambee hiyo.


Askofu Msonganzila akiwa katika picha ya pamoja na Nyangwine (wa nne kushoto) na wadau wengine wa maendeleo mara baada ya kiongozi huyo wa kiroho kuongoza ibada ya Jumapili katika Kanisa Katoliki Parokia ya Nyamwaga, kabla ya harambee hiyo kuanza.
-----------------------------------------------------
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages