NEWS

Sunday 3 December 2023

Wadau waunga mkono Right to Play, AICT uhamasishaji elimu kwa mtoto wa kike



Viongozi wakikabidhi kombe kwa washindi wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Matare wilayani Serengeti, hivi karibuni.
---------------------------------------------------

Na Waandishi wa Mara
Online News, Tarime
----------------------------------


Wanavijiji katika wilaya za Tarime na Serengeti wameendelea kufikiwa na kampeni ya uhamasishaji elimu bora kwa mtoto wa kike na iliyo jumuishi - inayoendeshwa na Shirika la Kimataifa la Right to Play kwa kushirikiana na Kanisa la African Inland Tanzania (AICT) Dayosisi ya Mara na Ukerewe.

Kampeni hiyo inaendeshwa sambamba na kupiga vita mila kandamizi na vitendo vya ukatili kwa mtoto wa kike, kupitia matamasha ya michezo mbalimbali kwa wanafunzi wa shule za msingi - kwa lengo la kuwaondolea wasichana vikwazo vya kupata elimu bora na kutimiza ndoto zao.



Kupitia matamasha hayo ya michezo, Right to Play inashirikiana na AICT kuwajengea wanafunzi, walimu na wazazi uwezo wa kusimamia misingi ya elimu bora na iliyo jumuishi.

Katika tamasha michezo lililofanyika hivi karibuni kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nyandage iliyopo kata ya Nyanungu – Tarime vijijini wanafunzi, walimu, wazazi na viongozi wa kijamii waliahidi kusambaza kwa watu wengine mafunzo waliyopata.

“Tunaomba matamasha kama haya yafanyike mara kwa mara ili wanafunzi hasa wa kike wasikatishwe masomo. Sisi tutasaidia kufikisha elimu hii kwenye shule nyingine,” alisema Afisa Elimu Kata ya Nyanungu, Mwl Petro Kimito.

Mthibiti Ubora wa Shule, Mwl Joseph Waryoba (wa pili kushoto), Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo (kushoto) na viongozi wengine wakijiandaa kukabidhi kombe kwa washindi wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi lililofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nyandage wilayani Tarime, hivi karibuni.
--------------------------------------------------------

Naye mkazi wa Kijiji cha Nyandage, Angelina Elias alisema “Tutafanyia kazi hii elimu tuliopata leo kutoka AICT na Right to Play, kwamba ni muhimu kuelimisha watoto wa kike, na tutaieleza jamii kwa upana kupitia mikutano ya kijiji.”

Mwanafunzi Maria Kisiri Chacha wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Nyandage yeye alisema tamasha hilo limekuwa na faida kubwa kwake kwani ameweza kujua madhara ya vitendo vya ukatili kwa watoto wa kike, vikiwemo vya ukeketaji na ndoa za utotoni.

“Nitakwemda kuwashauri watoto wenzangu wasome na siyo kukimbilia kuolewa wakiwa bado wadogo maana watapata madhara mengi ya kiafya,” alisema Maria.


Kwa upande wake Mthibiti Ubora wa Shule kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Mwl Joseph Waryoba alisema elimu ya kupinga ukatili ni kwa watoto wote, lakini mkazo zaidi unawekwa kwa watoto wa kike kwa sababu ndio wako hatarini zaidi ukilinganisha na watoto wa kiume.

“Watoto wa kike ndio tunawalenga zaidi na siyo kwamba tunawabagua wavulana, ila ni kwa sababu hizi mila kandamizi zinawaumiza zaidi watoto wa kike, hivyo tunapambana ili waondokane na matatizo hayo,” alisema Mwl Waryoba.


Mwl Waryoba akisisitiza jambo

Awali, akizungumza katika tamasha hilo, Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Daniel Fungo alisema wanashirikiana na Shirika la Right to Play kuendesha kampeni hiyo ili kuhakikisha kuwa jamii nzima inamthamini mtoto wa kike na kumpatia fursa sawa ya elimu bora kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Wasichana wengi wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na sababu nyingi katika jamii hasa za wafugaji ambazo zinamtazama mtoto wa kike kuwa kitega uchumi cha familia,hali inayomlazimu mtoto wa kike kukoswa fursa tofauti na alivyo mtoto wa kiume ambaye anapewa kipaumbele Zaidi katika familia.

Katika wilaya ya Serengeti, tamasha la michezo kwa wanafunzi wa shule za msingi Matare na Igina lilifanyika kwenye viwanjavya Shule ya Msingi Matare.



Emmanuel Saitot kutosha AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe alisisitiza kuwa kampeni hiyo ni muhimu kwa sababu inalengo kuwaondolea watoto wa kike vikwazo vya elimu vinavyochangia kuwakatisha masomo na kushindwa kufikia ndoto zao.

“Matamasha haya yanatoa fursa ya watoto kupata elimu na kueleza ndoto na changamoto zinazowakabili kuanzia kwenye familia zao,” alisema Saitot.

Mratibu wa Elimu Kata ya Matare wilayani Serengeti, Mwl Gisango Gabriel Mwita alilishukuru Shirika la Right to Play na AICT kwa juhudi hizo za kuisaidia Serikali kuhamasisha jamii kumpa mtoto wa kike fursa ya kupata elimu bora.

“Muda umefika sasa kwa jamii kubadilika na kuacha dhana potofu ya kumfanya mtoto wa kike kuwa kitega uchumi cha familia kwa kumwozesha katika umri mdogo, lakini pia tuacha vitendo vya ukatili wa kijinsia kama vile ukeketaji na vipigo,” alisema Mwl Mwita.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages