Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko (kulia) akizungumza na wanachama wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Zanzibar jana.
----------------------------------------------------
NA MWANDISHI WETU, Zanzibar
----------------------------------------------
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko ameitaka Jumuiya ya Wazazi ya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutumia rasilimali zake kukijenga na kukieneza chama hicho tawala katika maeneo mbalimbali nchini.
Pia ameitaka Jumuiya hiyo kuwaeleza wananchi kuhusu kazi kubwa za maendeleo ya kisekta zinazofanywa chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan.
Dkt Biteko ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Kundi la Wazazi), aliyasema hayo jana wakati akizungumza na viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Zanzibar, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Taifa, Dogo Mabrouk, katika kikao kilichofanyika kwenye Afisi Kuu ya CCM iliyopo Kisiwandui, wilaya ya Mjini mkoani Mjini Magharibi.
“Kama wewe ni Mwenyekiti wa Mkoa, Katibu wa Mkoa au kiongozi yoyote yule, kwa kutumia rasilimali ulizonazo - tembelea maeneo ya mkoa wako, wilaya na vijiji hata mara moja, zungumza na makundi mbalimbali ikiwemo Wajumbe wa Kamati za utekelezaji za Jumuiya yetu na waeleze kuhusu masuala ya kujenga na kueneza Chama.
“Hii inawezekana, tujipange, tufanye ziara hata kama ni kidogo, polepole tutafanya makubwa kadri tutakavyoendelea, tuwe mstari wa mbele kueleza mafanikio ambayo CCM na Serikali yake vimeyafanya,” alisisitiza Dkt Biteko.
Aliongeza kuwa Jumuiya ya Wazazi ni kubwa, hivyo inapaswa kufanya kazi za kukijenga chama hicho kwa kuwa inabeba makundi yote ndani ya CCM na haina mipaka au ukomo wa mtu kuwa sehemu ya Jumuiya.
“Nikitolea mfano Jumuiya ya Wanawake, inahusu wanawake katika Chama, Jumuiya ya Vijana umri fulani ukifika unakuwa hauna vigezo, lakini Jumuiya hii haina mipaka hivyo inapaswa kuwa na nguvu kubwa, tutumie ukubwa wa Jumuiya hii kuwasaidia Mwenyekiti wetu na Makamu Mwenyekiti upande wa Zanzibar katika kujenga Chama na kuzungumza kwa ukubwa yale yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika,” alisema.
Dkt Biteko (kushoto katikati) wakati wa ziara yake Zanzibar jana.
Naibu Waziri Mkuu huyo alisema Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt Samia na Makamu Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa Zanzibar, Dkt Ali Hussein Mwinyi wanataka kuona viongozi wa chama hicho katika ngazi mbalimbali wanawasaidia kazi, ikiwemo ya kueleza mafanikio makubwa ya kimaendeleo yanayoendelea kufanyika na kazi kubwa inayofanywa na viongozi hao katika kuwaunganisha Watanzania, kuwa na maridhiano na kujenga uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Mabrouk, alimshukuru Dkt Biteko kwa kuithamini Jumuiya hiyo na kuiwezesha kwa vitendea kazi ambavyo vitaboresha utendaji kwenye mikoa sita ya Zanzibar na kuahidi kuwa wataendelea kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.
Awali, kabla ya kikao hicho, Dkt Biteko alizuru katika kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume lililopo Kisiwandui, Zanzibar.
Aidha, Naibu Waziri Mkuu na Waziri huyo wa Nishati, alikabidhi pikipiki sita kwa ajili ya Jumuiya ya Wazazi (CCM) Zanzibar Pamoja na kofia ngumu kwa ajili ya Jumuiya hiyo kwenye mikoa sita ya Zanzibar.
Alisema pikipiki hizo ni mali ya Jumuiya ya Wazazi ambapo alielekeza zitumike kufanye kazi ya siasa kama ilivyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment