
Na Mwandishi Wetu
Rais Tharrnan Shanmugaratnam wa Singapore jana alianza ziara ya kiserikali Tanzania ikiwa na madumuni ya kuangalia maeneo muhimu ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Kiongozi huyo yupo Tanzania kwa ziara ya siku tatu kuanzia jana Jumanne kuzungumza na viongozi wa Tanzania na kuchambua sekta za ushirikiano kiuchumi.
Singapore ni moja ya mataifa ya Asia Kusini Mashariki ambayo kwa miongo ya hivi karibuni yamepiga hatua kwa na uchumi unaokua kwa kasi kuliko matarajio ya mataifa yaliyoendelea.
Utandawazi na mkazo mkubwa kwenye uzalishaji wa bidhaa zinazosafirishwa nje ni baadhi ya vitu vilivyoiwezesha nchi hiyo kuimarisha na kukuza uchumi wake.
Singapore siyo tu imekuwa tajiri kupitia biashara huria, bali pia nchi hiyo imekuwa mstari wa mbele kulinda viwanda vyake dhidi ya ushindani kutoka bidhaa za nje.
Rais Shanmugaratnam na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan, jana Jumanne walifanya mazungumzo yaliyolenga kutoa msukumo wa ushirikiano kiuchumi, kibiashara na uwekezaji kwa manufaa ya nchi zao.
Rais Samia alisema kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Singapore cha dola za Marekani milioni 299 bado ni cha chini kinachohitaji kuongezwa zaidi.
Hivi sasa Singapore inatekeleza miradi ya uwekezaji 36 nchini Tanzania ambayo baada ya kusainiwa kwa mkataba wa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili inabidi iongezeke maradufu.
Chini ya mkataba wa ushirikiano kiuchumi, Tanzania na Singapore zimeazimia kukuza sekta muhimu kama vile kilimo kuelekea kujitosheleza kwa chakula.
Katika mazungumzo yao, marais hao wawili walieleza wasiwasi wao kuhusu mabadiliko ya tabianchi ambayo walisema ni lazima hatua za haraka zichukuliwe kukabili tatizo hilo.
No comments:
Post a Comment