NEWS

Sunday 7 January 2024

Bodi ya Ushirika wa WAMACU inavyoendelea kuwa chachu ya huduma bora kwa wakulimaMwenyekiti wa Bodi ya WAMACU Ltd, David Mwita Hechei (kushoto) na GM Gisiboye wakifuatilia mada katika moja ya vikao vya Ushirika huo.
-----------------------------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU
----------------------------------------


BODI ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) ina kila sababu ya kujivunia mafanikio makubwa yaliyofikiwa ndani ya Ushirika huo katika kipindi kifupi cha miaka miwili, tofauti na awali ambapo ulikuwa haufahamiki vizuri kwa wakulima.

Rekodi zilizopo zinaonesha kuwa majukumu ya Ushirika huo yalikuwa hayatekelezwi ipasavyo, na kibaya zaidi ulifanya biashara kienyeji na kuwasababishia wakulima hasara.

Lakini tangu Bodi hiyo iingie madarakani mwaka 2020/2021, hudumza zimeendelea kuboreka siku hadi siku kwa ustawi wa wakulima katika mkoa wa Mara na halmashauri za Buchosa na Ukerewe mkoani Mwanza, ndani ya Kanda ya Ziwa Mashariki.

Maendeleo makubwa yameendelea kushuhudiwa ndani ya WAMACU Ltd, yakiakisi dira yake ya kuwa chama imara na endelevu - kinachokidhi mahitaji ya kiuchumi na kijamii kwa wanachama wake, yaani wakulima.

Bodi hiyo chini ya Mwenyekiti wake, David Mwita Hechei, imeonesha umahiri katika kusimamia dhima ya kuratibu na kuunganisha Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) kwa ajili ya kukusanya, kuhifadhi, kusindika, kutafuta masoko na kuuza mazao kwa tija.

Kwa sasa WAMACU Ltd inakusanya kahawa kwa kulipa fedha taslimu jambo ambalo linawafurahisha na kuwanufaisha wakulima, hasa kutokana na bei nzuri.

“Wakati Bodi hii inaingia madarakani Chama hiki kilikuwa kinakusanya na kuuza kahawa kienyeji, lakini kwa sasa kimejiimarisha katika huduma za pembejeo za kilimo zikiwemo mbolea na mbegu bora, lakini pia miche ya kahawa na huduma za ugani kwa wakulima.

“Pia sasa hivi Chama hiki kinahudumia hadi wakulima wa tumbaku katika wilaya za Serengeti na Rorya, tofauti na awali ambapo kilikuwa kinahudumia wakulima wa kahawa pekee,” alisema Meneja Mkuu (GM) wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye Marwa katika mahojiano maalum na Sauti ya Mara ofisini kwake juzi.

GM Gisiboye ambaye pia ni Katibu wa Bodi ya WAMACU Ltd, anataja siri ya mafanikio yote yanayoonekana ndani ya Ushirika huo kuwa ni uongozi mahiri wa Bodi hiyo ambayo ilikuja na mikakati endelevu iliyoanzisha na kuboresha huduma mbalimbali kwa wakulima.

Anatolea mfano huduma ya mbolea akisema imekuwa sehemu ya mafanikio makubwa katika kuutangaza Ushirika huo kibiashara, ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma kwa ubora wa hali ya juu.

Mafanikio mengine yanayoshuhudiwa ndani ya WAMACU Ltd ni pamoja na kupata uwakala wa TFRA na TOSCI kwa ajili ya kusambaza mbolea na mbegu bora kwa wakulima.

“Lakini pia tumefanikiwa kuongeza idadi ya wafanyakazi kutoka wawili tuliowakuta hadi 40 wa kuajiriwa na vibarua zaidi ya 60,” anaongeza GM Gisiboye.

Anasema wafanyakazi hao wanasaidia urahisishaji wa shughuli za kusambaza mbolea na mbegu kwa wakulima, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kiwanda cha kukoboa kahawa inayokusanywa na WAMACU Ltd kupitia AMCOS.

“Hatua hii imechangia mafanikio ya kahawa yetu aina ya Arabica kuendelea kung’ara katika mashindano ya kahawa bora ndani na nje nchi kuanzia msimu wa mwaka 2021/2022 na 2022/2023,” anasema GM Gisiboye na kuongeza:

“Aidha, kahawa ya Tarime ilishinda katika shindano la muonjo na kupata Tuzo ya Tanzania Fine Coffee Competition kwenye kipengele cha kahawa ngumu isiyooshwa, na pia tulifanikiwa kuwa wa pili kwenye kipengele cha kahawa ngumu ya kuoshwa.”

Inakumbukwa pia kwamba kahawa inayozalishwa Tarime mkoani Mara inaongoza kwa kuuzwa kwa bei nzuri katika soko la minada ikilinganishwa na kahawa ya maeneo mengine nchini.


Kahawa aina ya Arabica inayozalishwa wilayani Tarime inatamba kwa ubora katika soko la dunia.
-------------------------------------------------
WAMACU Ltd pia inaendelea kuwezesha mafunzo ya matumizi bora ya mbolea kwa wakulima na kusaidia utoaji wa mafunzo ya mfumo wa MUVU.

Vilevile imefanikiwa kuagiza mashine za kuchakata kahawa kavu na kahawa mbivu, ambapo kwa sasa mitambo inaendelea kufungwa na wahandisi husika. Hivyo haitakodi wala kugharimika kwenye ukoboaji kahawa jambo ambalo litaipunguzia mzigo wa uendeshaji na hatimaye kuleta manufaa kwa wakulima.

Pia kwa sasa WAMACU Ltd ina ofisi ya kuhudumia wakulima tofauti na zamani ambapo ilikuwa inalazimika kutumia maghala ya mazao.

Chini ya uongozi wa Bodi ya WAMACU Ltd, Chama hicho pia kimefanikiwa kurudishiwa na kuthaminisha mali zilizokuwa chini ya ufilisi za iliyokuwa Mara Cooperative Union (MCU (1984) Ltd).

GM Gisiboye anataja mafanikio mengine ya WAMACU Ltd kuwa ni uwekezaji wa vituo vya mafuta katika kiwanja kilichopo Nyangoto na cha Ushirika huo mjini Tarime.

Chama hicho pia kimeanzisha huduma ya Wakala wa Benki ya NMB, ikiwa utekelezaji wa agizo la Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC).

Kwa mujibu wa GM Gisiboye, Bodi ya WAMACU Ltd imefanikiwa kuleta maendeleo hayo yote kutokana na ushirikiano ambao Chama hicho kinapata kutoka serikalini.

Anasema Bodi hiyo inaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa chachu ya maendeleo ya Ushirika huo.

Anataja Wizara ya Kilimo inayoongozwa na Hussein Bashe, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), viongozi wa Kilimo Kanda ya Ziwa, mkoa wa Mara na wilaya ya Tarime kama mihimili mikuu ya shughuli za maendeleo ya WAMACU Ltd.

Hata hivyo, GM Gisiboye anasema pamoja na changamoto nyingine, Ushirika huo hauna gari la kusafirisha mbolea na kahawa kwenda, au kutoka kwenye AMCOS hali inayoulazimu kukodi magari ya watu binafsi kwa gharama kubwa.

Anataja mikakati ya WAMACU Ltd kuwa ni pamoja na kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), INTRACOM, TFC, OPC, MIJINGU na kampuni nyinyine kwa ajili ya kusambaza mbolea ya ruzuku kwa wakulima katika halmashauri za Tarime, Bunda Butiama, Rorya, Serengeti na Musoma.

“Chama pia kiko kwenye hatua za mwisho za ukamilishaji wa mpango wa biashara ya mahindi kwa ajili ya kuanza ukusanyaji, uchakataji na ufuatiliaji wa masoko makubwa ya mahindi katika ukanda wa Tarime.

“Aidha, WAMACU Ltd itaendelea kupokea na kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kadri yatakavyotolewa ili kukidhi mahitaji ya kumhudumia mkulima pembejeo za kilimo,” anasema GM Gisiboye.

Anataja mikakati mingine kuwa ni kuongeza jitihada za ukusanyaji wa kahawa ili kupata ziada kubwa na kumwezesha mkulima kunufaika na malipo ya pili.

Bila kusahau kusimika viwanda vya kuchakata kahawa mbivu pamoja na kuwa na kiwanda kikubwa cha kuchakata kahawa za aina zote na kuendeleza mfumo wa stakabadhi ghalani kwa lengo la kumwezesha mkulima kulima kwa tija, huku akipokea malipo yake kwa taslimu.

Si hayo tu, WAMACU Ltd pia ina mkakati wa kuongeza na kusajili wanachama wapya, yaani AMCOS, mashirika na taasisi binafsi, na watu wenye mashamba makubwa.

Mikakati mingine ni kuendelea kuhamasisha wakulima kujiandikisha kupitia maafisa kilimo ili waweze kupata namba za siri za kununua mbolea ya ruzuku ya Serikali.

Pia kuendelea kutafuta soko la kahawa la moja kwa moja nje ya nchi kupitia kampuni tanzu zilizopo nchini kwa ajili ya kupata bei kubwa ya kumnufaisha mkulima. “Tayari tuna leseni ya kuuza kahawa moja kwa moja na tumeanza kufuatilia njia mbalimbali za kusafirisha mzigo wa mteja mpaka Ulaya,” anasema GM Gisiboye.

Meneja Mkuu huyo wa WAMACU Ltd anawapa wakulima matumaini zaidi kwamba wategemee kuendelea kupata huduma bora za pembejeo na masoko yenye tija kupitia Ushirika huo.

“Tunatoa wito kwa wakulima kuendelea kutupatia ushirikiano na kutuunga mkono kwa kutumia huduma zetu kwa kupata mbolea na mbegu,” anasema GM Gisiboye na kuwataka wakulima kujiepusha na matumizi ya pembejeo kutoka nje ya Tanzania.

Aidha, anawahimiza wakulima kuendelea kukusanya na kuuza mazao yao kupitia WAMACU Ltd ili kupata malipo ya pili na kuwa huru kutembelea ofisi za Ushirika huo ili kupata maelekezo na huduma wanazohitaji.

“Matarajio yetu ni kwamba Serikali itaendelea kutuunga mkono ili nasi tuendelee kuhudumia wakulima kwa weledi wa hali ya juu,” anasema GM Gisiboye.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages