NEWS

Sunday 14 January 2024

Dkt Nyansaho azuru banda la TANAPA kwenye Maonesho ya 10 ya Biashara ya Kimataifa Zanzibar



Dkt Rhimo Simeon Nyansaho (wa tatu kutoka kushoto) na wengine wakifurahia picha ya pamoja katika banda la TANAPA kisiwani Zanzibar leo.
-----------------------------------------------------

Na Zainab Ally, Zanzibar
----------------------------------


MWENYEKITI wa Bodi ya TANESCO na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Dkt Rhimo Simeon Nyansaho, ameeleza kuridhishwa na utendaji wa kazi unaofanywa na shirika hilo katika kulinda maliasili na kukuza utalii unaoliongezea taifa mapato.

“Nimeridhishwa na kufurahishwa na utendaji kazi wa TANAPA kwani juhudi zenu naziona na zimekuwa na matunda chanya ambayo yameendelea kuliongezea taifa mapato,” amesema.

Dkt Nyansaho ameyasema hayo leo Jumapili wakati alipotembelea banda la TANAPA wanaoshiriki Maonesho ya 10 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika Jimbo la Kiembe Samaki - Fumba, Zanzibar.

Amewataka TANAPA waendelee na juhudi za kutangaza Hifadhi za Taifa, lakini pia kuitangaza Nyumba ya Kumbukizi ya Mwl Nyerere iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam, ili iwajengee watoto uzalendo wa kuipenda nchi yao.

Aidha, ameshauri pawepo na gari maalum la kuwachukua wanafunzi kutoka shuleni kuwapeleka katika nyumba hiyo Mwl Nyerere kwa ajili ya kufundishwa kuyaishi aliyoyaishi Baba huyo wa Taifa wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.

Akimkaribisha Mjumbe huyo wa Bodi ya Wadhamini katika banda la TANAPA, Afisa Mwandamizi kutoka Kitengo cha Utalii - Hifadhi ya Taifa Mikumi, Herman Baltazary amesema lengo la kushiriki Maonesho ya 10 ya Biashara ya Kimataifa ni kuzitangaza Hifadhi za Taifa na fursa za uwekezaji zinazopatikana ndani ya hifadhi hizo.

Baltazary ameongeza kuwa kutokana na unyeti wa maonesho hayo, pia imekuwa ni fursa nzuri ya kuonana na wadau wa utalii, wakala wa usafirishaji na waongoza utalii ili kujenga mahusiano mazuri.

Amesema mahusiano hayo yatasaidia wakati wanapouza fukwe kwa wageni wao wawe na vifurushi pia vya kuvinadi vivutio vya utalii vinavyopatikana ndani ya Hifadhi za Taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages