
Mbunge wa jimbo la Serengeti, Mary Daniel Surati, akizungumza Bungeni jijini Dodoma.
Dodoma
-----------------
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Surati, ameitaka Wizara ya Kilimo kutafuta suluhu ya maji ya Mto Mara kuvamia mashamba na makazi ya wananchi katika kata ya Kisaka.
“Kwa niaba ya wananchi wangu wa Serengeti, ni lini serekali itatatua changamoto ya Mto Mara, hasa kwenye eneo la kata ya Kisaka ambapo maji yanaacha njia yake na kuvamia maeneo ya kilimo na makazi ya wananchi,” Mbunge Mary alihoji wiki iliyopita wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwenye mkutano wa Bunge unaoendelea jijini Dodoma.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, alisema mbali na kufanya ziara katika jimbo la Serengeti kuangalia tatizo hilo, atatuma wataalamu wa wizara hiyo kutafuta suluhu.
“Wizara ya kilimo sisi ni watu ambao tunaweza kutembea na kufika maeneo yote, kwa hiyo nitafika kwenye eneo ambalo umeliainisha, lakini tutatuma wataalamu kuhakikisha tunaondoa hiyo adha mara moja,” Silinde alimhakikishia mbunge huyo kijana wa jimbo la Serengeti.
Mto Mara unaanzia Milima ya Mau nchini Kenya na kupita katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kabla kutiririsha maji ndani ya Ziwa Victoria upande wa Tanzania.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment