NEWS

Friday 26 January 2024

Kamishna wa Uhifadhi TANAPA aagiza maeneo ya barabara yaliyoharibika Hifadhi ya Serengeti yarekebishwe haraka



Kamishna wa Uhifadhi (CC) wa TANAPA, Juma Kuji (kulia) akizungumza na wasaidizi wake alipokwenda kukagua miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua katika Hifadhi ya Taifa Serengeti jana.
----------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Serengeti
--------------------------------------------


KAMISHNA wa Uhifadhi (CC) wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Juma Kuji ameiagiza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kurekebisha haraka maeneo ya barabara yaliyoharibika ndani ya hifadhi hiyo.

CC Kuji alitoa agizo hilo jana alipofanya ziara ya kukagua miundombinu ya barabara, akifuatana na Mkuu wa Hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Moronda Moronda.

Alisema maboresho ya miundombinu ya barabara katika Hifadhi ya Taifa Serengeti ni muhimu kwa ajili ya kuwezesha wageni kuitembelea bila kikwazo.



“Licha ya mvua kubwa zinazoendelea hatuwezi kusubiri ziishe, tumeazimia kushughulikia kwa haraka maeneo yote korofi, ikiwa ni hatua za haraka… lengo kuu ni kuhakikisha barabara hizi zinakuwa na tabaka gumu. Haya ni maagizo yangu kwa Menejimenti kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote,” alisema CC Kuji.

Alitumia nafasi hiyo pia kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya barabara za hifadhi - iliyoathiriwa na mvua.

Alisema TANAPA imejipanga kuhakikisha kuwa miundombinu ya barabara zote katika Hifadhi za Taifa Tanzania inaboreshwa, ili kukidhi matamanio ya wageni wanaozitembelea kujionea na kufurahia vivutio lukuki vya utalii.



Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia miundombinu, Mhandisi Dkt Richard Matolo alisema TANAPA imekuwa ikitumia teknolojia mbalimbali kutafuta ufumbuzi wa changamoto za barabara zake.

“Shirika limefanya majaribio mbalimbali na kuja na teknolojia ambazo zitafanya barabara hizi, hususan hii ya Naabi iwe inapitika wakati wote. Imethibitika kuwa tunaweza kutumia tabaka gumu kujenga barabara hizi,” alisema Mhandisi Matolo.

Akikazia hoja hiyo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Moronda, alisema Menejimenti imejipanga kuhakikisha kuwa maeneo yaliyoharibika yanarekebishwa haraka iwezekanavyo.

Moronda alitoa rai ya kuwakumbusha waongoza watalii kuzingatia sheria na taratibu za hifadhi, ikiwemo alama za barababrani ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza, hasa kipindi hiki cha mvua.



Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Mkuu anayeshughulikia Mawasiliano TANAPA, Catherine Mbena alisema: “Lengo letu kama Shirika ni kuhakikisha wageni wetu [watalii] wanapofika maeneo yetu wanaondoka na kumbukumbu nzuri, ndio maana timu ya TANAPA iko hapa kuhakikisha kipande hiki korofi kinapitika.

Aliongeza: “Tumekuwa na mipango ya muda mrefu na mfupi mrefu, na yote tutaitekeleza, lengo likiwa ni wageni wetu wafurahie vivutio hivi vya kipekee duniani.”

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages