NEWS

Monday 29 January 2024

Makamu wa Rais Dkt Mpango awasihi vijana kutokubali kutumiwa na wanasiasa kuchochea vurugu



Mkamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Philip Mpango akihutubia wakati wa Kongamano la UVCCM kwenye Uwanja wa Kawawa mkoani Kigoma jana,
------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
--------------------------------------------

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Philip Mpango amewataka vijana kutokukubali kutumiwa na wanasiasa kuchochea vurugu, uhasama na maandamano yasiyo na tija kwa Taifa.

Dkt Mpango ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alituma ujumbe huo wakati wa Kongamano la Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) kuelekea Miaka Mitatu ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan madarakani na Miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM, lililofanyika Uwanja wa Kawawa mkoani Kigoma jana.

Aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea maslahi ya Taifa pamoja na kutumia ushawishi wao kuwahimiza vijana wengine na watu wazima kuendelea kukiunga mkono chama hicho tawala kwa kuwaonesha mafanikio makubwa yaliyofikiwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt Samia.

Aidha, Dkt Mpango aliwataka wanachama wa UVCCM kuendelea kuungana na kushikamana ili kujenga Jumuiya iliyo bora na yenye nguvu.

Alisema UVCCM kama zilivyo jumuiya nyingine za chama hicho ni muhimu katika kuimarisha CCM, hivyo inapaswa kubaki katika umoja wake, kwa kuepuka kutengeneza makundi, majungu, matamko ya vitisho na kauli zisizofaa.


Makamu wa Rais Dkt Mpango akisalimiana na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Ali Kawaida wakati alipowasili katika kongamano la umoja huo mkoani Kigoma.
--------------------------------------------
Kiongozi huyo alihimiza vijana kutambua adhma ya Rais Dkt Samia katika kujenga demokrasia na kuimarisha utawala unaojali maslahi ya umma, ili kujenga ustahimilivu kwa kuepuka migongano, kutafuta suluhu na mapatano pale kunapotokea kutoelewana, na hivyo kuleta mageuzi yatakayochochea ustawi wa Taifa.

Pia alitoa wito wa kuhamasisha vijana kuuthamini na kuulinda kwa nguvu zote Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania, kwa kukemea wanasiasa ambao wamekuwa wakitoa kauli zenye mwelekeo wa kubeza mafanikio ya Muungano huo.

Halikadhalika, Dkt Mpango aliendelea kuwahimiza vijana wa CCM kuwa kielelezo cha uadilifu, kufanyakazi kwa bidii na kuishi kwa kuzingatia sheria za nchi, mila na desturi zilizopo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatumia mitandao ya kijamii vizuri ili kujipatia maarifa.

Alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kutumia fursa ya maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kushiriki mijadala yenye tija - inayolenga kutafuta ufumbuzi wa matatizo katika jamii.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais Dkt Mpango amewataka vijana nchini kushiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Alifafanua kuwa ushiriki huo ni pamoja na kupanda na kutunza miti, na kusaidia kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira, ikiwemo uchomaji moto ovyo.

Sambamba na hilo, aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza matumizi ya nishati mbadala ya kupikia, ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yameendelea kuwa makubwa na kusababisha upotevu mkubwa wa misitu nchini.

Katika Kongamano hilo, mafanikio mbalimbali ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia yalianishwa, yakiwemo katika sekta za afya, kilimo, maji, elimu, nishati na miundombinu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages