NEWS

Sunday 14 January 2024

Rais Samia awalilia wachimbaji wadogo waliokufa kwa kufunikwa na kifusi ngodini Simiyu



Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
----------------------------------------

NA MWANDISHI WETU
----------------------------------

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa wachimbaji wadogo zaidi ya 20 waliopoteza maisha kwa kufunikwa na kifusi katika mgodi wa dhahabu wa Ng’alita katika wilaya ya Barriadi, mkoani Simiyu.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu zaidi ya 21 kufuatia ajali ya kufunikwa na ardhi katika Mgodi wa Ng'alita. Ndugu zetu hawa walikuwa wachimbaji wadogo katika eneo hili, wakijitafutia riziki zao, familia zao na kuchangia maendeleo ya taifa letu.

“Natuma salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza jamaa zao katika ajali hii. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vikishirikiana na uongozi wa mkoa vinaendelea na juhudi za kutafuta miili mingine ambayo bado imekwama ndani ya kifusi,” amesema Rais Samia katika sehemu ya salamu hizo za pole alizotuma leo Jumapili.

Wakati huo huo, Serikali imeamua kuufunga mgodi huo wa Ng’alita ili kupisha uboreshaji wa miundombinu kwenye eneo hilo.

“Baada ya ukaguzi wa eneo, tumegundua kwamba kulikuwa na ukosefu wa miundombinu inayofaa kwa usalama kwa shughuli za uchimbaji kama sheria ya madini inavyotamka,” amesema Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt Yahaya Nawanda katika mahojiano na redio ya TBC Taifa.

Vifo vya wachimbaji hao vilitokea katika mgodi huo uliopo kijiji cha Ikinabushu kilichoko kata ya Gilya na tarafa ya Dutwa, ambako wachimbaji zaidi ya 3,000 walikwenda kutafuta utajiri kutokana na madini ya dhahabu.

Inaaminika kwamba mvua zinazoendelea kunyesha katika eneo hilo pamoja na maeneo mengine ya Tanzania, huenda zilisababisha kifusi kushuka na kuwafunika wachimbaji walipokuwa kwenye shughuli zao.

Katika miaka ya hivi karibuni, majanga katika sektsa ya madini yamekuwa ni matukio ya mara kwa mara, baada ya kutanuka kwa sekta ya madini kufuatia ujio wa uchumi huria tangu miaka ya 1980.

Kwa kiasi kikubwa kukua kwa sekta ya madini kunachangia ongezeko la pato la taifa, ambapo kufikia mwakani mchango wa sekta hiyo unatarjiwa kufikia asilimia 10, kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages