NEWS

Monday 1 January 2024

Serikali wilayani Tarime yataka vyanzo vya maji vipimwe na kupata hatimilikiKatibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl Saul Mwaisenye, akihutubia mkutano wa mwaka wa wadau wa maji wilayani humo, Ijumaa iliyopita. (Picha na Sauti ya Mara)
---------------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Tarime
---------------------------------------------


SERIKALI wilayani Tarime imeziagiza mamlaka za vijiji na wadau husika kushughulikia upimaji wa maeneo ya vyanzo vya maji ili yapate hatimiliki.

Hatua hiyo itasaidia kuepusha uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji na miundombinu yake katika wilaya hiyo ya mkoani Mara.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Tarime, Mwl Saul Mwaisenye aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, Kanali Michael Mntenjele katika mkutano wa mwaka wa wadau wa maji wilayani hapa, Ijumaa iliyopita.Mkutano huo uliandaliwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tarime, ukiwashirikisha watumishi wa taasisi za maji na mazingira, viongozi wa kata, vijiji na jumuiya za watumia maji.

DAS Mwaisenye alitumia nafasi hiyo pia kuwahimiza viongozi wa ngazi za vijiji, mitaa na kata kuhamasisha wananchi kushiriki katika ulinzi na utunzaji wa vyanzo vya maji na miundombinu yake.

Huku akiipongeza RUWASA kwa kazi nzuri, kiongozi huyo aliwataka wateja kuhakikisha wanalipa bili za maji kwa wakati ili kuwezesha huduma hiyo kuwa endelevu.

Kwa upande mwingine, alizitaka mamlaka za maji kudai malipo halisi bila kuwabambikia wateja bili za maji. “Ni kinyume cha sheria kumdai mtu kitu ambacho hajakitumia,” alisema.


Afisa Ufuatiliaji, Tathmini na Mafunzo kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) Mkoani Mara, Enock Edward Rutaihwa alisema wanaendelea kuwezesha jamii kutunza vyanzo vya maji na misitu.

“Pamoja na majukumu mengine, WWF tunahamasisha ushirikishaji jamii katika usimamizi wa vyanzo vya maji na miundombinu yake,” alisema Rutaihwa.

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama tawala - CCM Wilaya ya Tarime, Marema Solo, mbali na kuishukuru RUWASA kwa kuboresha huduma ya maji, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha za utekelezaji wa miradi ya maji wilayani hapa.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages