NEWS

Wednesday 3 January 2024

TAWA: Uwindaji wa mamba mkubwa nchini ulizingatia sheria



Mwindaji akifurahia kufanikisha uwindaji wa mamba mkubwa nchini, hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
----------------------------


MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imekamilisha uchunguzi na kutoa ufafanuzi kuhusu picha jongefu (video clip) iliyosambazwa kwenye mtandao wa kijamii hivi karibuni, inayoonesha mtu akishangilia kufanikisha uwindaji wa mamba mkuwa nchini mwenye rekodi ya dunia.

Katika taarifa yake kwa umma iliyoitoa juzi Jumanne, TAWA ilisema mamba huyo aliwindwa katika kitalu cha Lake Rukwa GR kwa kibali halali namba MP-0001792 kilichoanza Agosti 12 hadi Septemba 9, 2023.

“Mamba huyo alikuwa na urefu wa futi 16.2 sawa na sentimita 493.8 ikiwa ni juu ya kiwango cha chini cha urefu wa sentimita 300 unaohitajika kwa mujibu wa sheria,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo ya TAWA na kuendelea:

“Vilevile, kumbukumbu zinaonesha, uwindaji huu ulisimamiwa na askari kutoka TAWA na mwindaji bingwa kutoka kwenye kampuni iliyopewa kibali kwa mujibu wa sheria. Aidha, ada na tozo zote zinazohusiana na uwindaji wa mamba zililipwa kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia uwindaji hapa nchini.

“Wakati uwindaji ukifanyika askari anayesimamia uwindaji huhakikisha uwindaji unafanyika kwa kuzingatia sheria na kulinda usalama wa wageni wawindaji na watu walioambatana nao. Hivyo taratibu zote hizi za kisheria zilizingatiwa na hakuna utaratibu uliokiukwa.”

Awali, wakati TAWA ikitangaza kufanya uchunguzi wa tukio hilo, iliweka hadharani masharti ya uwindaji wa kitalii wa mamba chini ya Kanuni na Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyo hatarini kutoweka (CITES).

Mamlaka hiyo ilitaja masharti ya uwindaji wa mamba chini ya kanuni na mkataba huo ambao Tanzania imeuridhia, kuwa ni kuhakikisha idadi ya mamba wanaowindwa nchini hawazidi 1,600 kwa mwaka, na kila mmoja awe na urefu usiopungua sentimita 300.

Masharti mengine ni vibandiko maalum kufungwa kwenye ngozi za mamba wanaowindwa, na wawindaji lazima wawe na vibali vya CITES vinavyotumika kusafirisha nyara za wanyamapori hao.

Kwa mujibu wa TAWA, mamba ni miongoni mwa wanyamapori wanaolindwa na Mkataba wa CITES, na wamewekwa katika kundi la pili linaloruhusu matumizi ya uvunaji, ikiwemo uwindaji wa kitalii.

Chini ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania na Mkataba wa CITES, mtu yeyote anaruhusiwa kufanya uwindaji wa kitalii baada ya kupata kibali kutoka TAWA ambayo pia ina wajibu wa kusimamia uwindaji huo katika hatua zake zote.

“Kumbukumbu tulizo nazo zinaonesha kuwepo kwa vibali vya uwindaji wa wanyamapori wakiwemo mamba katika maeneo mbalimbali nchini,” ilieleza TAWA.

Tanzania ndiyo nchi pekee barani Afrika iliyojizolea sifa ya kuwa na eneo zuri la kuwaona mamba, na inakadiriwa kuwa na asilimia 50 ya mamba 600,000 wanaopatikana Afrika.

Taifa hili kubwa la Afrika Mashariki limejaliwa kuwa na maziwa na mito mingi ambayo ni makazi asilia kwa ustawi wa mamba.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages