NEWS

Saturday 24 February 2024

AICT, Right to Play wasisitiza elimu bora kwa watoto wenye ulemavu, mahitaji maalumu



Afisa Mtendaji Kata ya Itiryo, Pendo Mushi akikabidhi kombe kwa mwakilishi wa timu iliyoshinda katika tamasha la michezo lililoandaliwa na AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Right to Play kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Itiryo, wilayani Tarime jana.
------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
--------------------------------------


KANISA Africa Inland Tanzania (AICT) Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Right to Play, wameendelea kuhimiza jamii kuwapa watoto wenye ulemavu na mahitaji maalumu haki zote za msingi, ikiwemo ya kupata elimu bora.

Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo alisisitiza hayo alipozungumza na wazazi, walimu na wanafunzi wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Itiryo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, Februari 23, 2024.


Wanafunzi wakicheza igizo wakati wa tamasha hilo
------------------------------------
“Kama huko majumbani kuna watoto wenye alemavu, au wenye mahitaji maalumu na hawajapelekwa shule, mtoe taarifa kwa uongozi na sisi [AICT na Right to Play] tutafuatilia taarifa hiyo ili waweze kupata elimu, kwa sababu elimu ni haki ya kila mtoto,” alisema Fungo.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Itiryo, Pendo Mushi aliwashukuru AICT na Right to Play na kuwataka wanafunzi kuwa mabalozi wazuri wa kusambaza ujumbe huo kwa jamii nzima.

“Ninyi wanafunzi muwe mabalozi na waelimishaji kwamba mtoto mwenye ulemavu akipata elimu anaweza kuwa mtendaji, daktari au hata rais. Kwa hiyo na wao wana haki ya kupata elimu. Lakini pia wale waliofichwa mkatusaidie kutoa taarifa ili wasaidiwe kupata haki yao ya msingi,” alisema Mushi.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Itiryo, Shadrack Julius alisema: “Tunawashukuru sana AICT na Right to Play kwa sababu mbali na elimu, pia wametupatia darasa na linatusaidia sana, hivyo niwaombe muendelee kuja mara kwa mara maana kuja kwenu kuna manufaa sana kwetu.”


Afisa Mtendaji wa Kata, pendo Mushi akizungumza. Kushoto ni Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo.
------------------------------------
Nao wanafunzi wa shule hiyo walizishukuru taasisi hizo na kuwaomba wazazi kutowaficha watoto wenye ulemavu na kuwanyma elimu.

“Wazazi wawapeleke shule watoto wao wenye ulemavu, wasiwafiche maana elimu ni ufunguo wa maisha,” alisema Rhobi Daniel Marwa, mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Itiryo.

Right to Play na AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe wamekuwa wakishirikiana kuendesha mradi wa elimu bora na iliyo jumuishi kwa kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi kupitia matamasha ya michezo, midahalo na semina mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages