NEWS

Friday 23 February 2024

Polisi Tarime Rorya wamtia mbaroni Mwenyekiti wa Kitongoji anayetuhumiwa kumshambulia mwanamke kikatili



RPC Tarime Rorya, Mark Njera.
------------------------------------------

Na Mwandishi wa Mara
Online News, Tarime
--------------------------------


JESHI la Polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya linamshikilia Menyekiti wa Kitongoji cha Majengo Mapya Silas Nguka Nyamhanga (46), anayetuhumiwa kumshambulia mwanamke kikatili.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Mark Njera, upelelezi wa shauri hilo umekamilika na jalada limepelekwa kwa Wakili wa Serikali kwa ajili ya kuandaa mashtaka ili mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani.

RPC Njera amesema askari polisi walimkamata Nyamhanga kufuatia video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha mwanamke (jina tunalihifadhi) mkazi wa Nyamongo akiugulia maumivu ya majeraha aliyopata sehemu mbalimbali za mwili wake, huku msimulizi wa video hiyo akieleza kuwa mwanamke huyo alifanyiwa ukatili wa kupigwa kwa rungu na mwenyekiti huyo wa kitongoji.

“Tukio hili liliripotiwa Februari 17, 2024, ambapo mwanamke huyo (akimtaja jina) mwenye umri wa miaka 31, mhudumu wa baa iitwayo Chimbo Pub iliyopo katika kitongoji cha Nyangoto, kijiji cha Nyangoto, kata ya Matongo, alijeruhiwa kwa kushambuliwa kwa kupigwa na rungu, ngumi na mateke sehemu mbalimbali za mwili wake - hali iliyosababisha kung'oka meno mawili na jino moja kupasuka.

“Chanzo cha tukio hilo ni mtuhumiwa [Nyamhanga] kudaiwa pesa kiasi cha shilingi 24,000 alizokunywa pombe katika baa hiyo, ambapo mtuhumiwa alimhadaa mwanamke huyo na kumpeleka nyumbani kwake ili akamlipe pesa hiyo, badala yake alimfungia ndani ya uzio na kuanza kumshambulia.

“Katika nyumba hiyo alikuwepo mke wa mtuhumiwa na kijana wake wa kiume ambaye ndiye aliyefungua mlango wa geti na mwanamke huyo kupata nafasi ya kukimbia.

“Mlalamikakaji alipatiwa PF.3 (Fomu Namba 3 ya Polisi) kwa ajili ya matibabu, na hali yake inaendelea vizuri,” imeeleza taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi.

Kufuatia tukio hilo, RPC Njera ameendelea kutoa wito wa kuhimiza wananchi wote katika Mkoa wa Polisi Tarime Rorya kujiepusha na vitendo vya ukatili, la sivyo watashukiwa na rungu la dola kwani vitendo hivyo vina athari kubwa kwa jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages