Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa.
-----------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Mara
------------------------------------
MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa, akimtaja kama kiongozi aliyetumikia taifa la Tanzania kwa bidii na uaminifu.
“Tumepoteza kiongozi wetu ambaye alikuwa mchapakazi na mwenye maono, na alilitumikia taifa letu vizuri katika sekta mbalimbali, ikiwemo kuweka msukumo wa ujenzi wa shule za kata,” Chandi aliliambia Gazeti la Sauti ya Mara juzi, saa chache baada ya kifo cha Lowassa kutangazwa na Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango.
Chandi alituma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas Ole Sabaya, wananachi wa jimbo la Monduli na Watanzania wote kufuatia kifo hicho cha Lowassa - ambaye mbali ya kuwa Waziri Mkuu, amewahi kuwa waziri katika wizara mbalimbali.
“Natoa pole kwa familia ya Mzee Lowassa, ndugu, wananchi wa Monduli na Watanzania wote kutokana na msiba huu mkubwa,” alisema kiongozi huyo wa CCM Mara, huku akibainisha kuwa Lowassa alikuwa rafiki yake wa karibu.
Edward Ngoyai Lowassa enzi za uhai
-------------------------------------------------
Tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi na kutangaza siku tano za maombolezo nchini, huku bendera zikipepea nusu mlingoti.
Nacho Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kimetuma salamu za rambirambi kufuatia kifo hicho cha Lowassa ambaye pia ni Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Monduli mkoani Arusha.
“Chama Cha Mapinduzi kitamkumbuka ndugu Edward Ngoyai Lowassa kwa umahiri na uzalendo katika kukitumikia chama hicho na taifa kwa ujumla, akitumia elimu na uzoefu wake kwa maslahi mapana ya Chama, Serikali na Bunge,” ilisema sehemu ya taarifa ya salamu za rambirambi iliyosainiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda.
Lowassa alifariki dunia juzi Februari 10, 2024 jijini Dar es Salaam akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikokuwa akipata matibabu ya maradhi ya mapafu na shinikizo la damu.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment