Rais wa Hungary, Katalin Novak (pichani) amejiuzulu wadhifa huo.
Novak alitangaza hatua hiyo juzi Jumamosi jioni, kupitia kipindi cha moja kwa moja kwenye televisheni, kufuatia uamuzi wake wa kumsamehe mtu ambaye alikuwa amepatikana na hatia ya kuficha kesi ya unyanyasaji watoto kingono.
Kujiuzulu kwa Novak kulifuatia maandamano ya raia wa nchi hiyo ya Ulaya kuhusu uamuzi wake wa kumsamehe afisa ambaye alikuwa amefungwa jela kwa kuwalazimisha watoto kufuta madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya mkurugenzi wa makao ya watoto yanayosimamiwa na serikali.
Wakati akitoa hotuba yake moja kwa moja kwenye televisheni, Kovak alisema alitoa msamaha huo kwa imani kuwa mwanaume aliyehukumiwa hakutumia vibaya udhaifu wa watoto waliokuwa chini ya uangalizi wake.
Alikubali kosa lake na akaomba radhi kwa kutoa msamaha huo. “Nilifanya makosa, kwani msamaha na ukosefu wa hoja ulisaidia kuzua mashaka,” Novak alisema.
Mzozo uliosababisha kujiuzulu ulikuja baada ya majina ya watu 25 waliosamehewa na Novak Aprili mwaka jana, kama sehemu ya ziara ya Papa Francis nchini Hungary, kuwekwa hadharani na vyombo vya habari vya Hungary hivi karibuni.
Katika orodha ya wafungwa kulikuwa na naibu mkurugenzi wa makao ya watoto karibu na Budapest, ambaye alikuwa jela kwa miaka mitatu tayari baada ya kuwalazimisha watoto kufuta madai ya unyanyasaji dhidi ya mkurugenzi wa nyumba hiyo.
Mkurugenzi huyo alikuwa amefungwa jela kwa miaka minane kwa kosa la kuwadhulumu watoto katika kituo hicho kinachosimamiwa na serikali.
Vyama vya upinzani vya Hungary na waandamanaji walikuwa wakimtaka ajiuzulu, lakini uamuzi wa Novak kufanya hivyo ulikuwa wa ghafla kama vile haukutarajiwa.
“Leo nimejiuzulu kutoka ofisi yangu kama Rais wa Hungary. Asante kwa kila kitu marafiki zangu wote katika pembe zote nne za dunia.
“Hungary ni nchi nzuri yenye watu wazuri, mshirika mzuri, rafiki bora na mshirika anayetegemeka. Nina furaha kwamba katika miaka iliyopita ningeweza kufanya kazi ili kuhamasisha watu kuhusu hili duniani,” Novak alisema kupitia Twitter.
Judit Varga, waziri wa zamani wa sheria aliyeidhinisha msamaha huo, pia amejiuzulu nafasi yake mpya ya kuongoza kampeni za uchaguzi wa Ulaya kwa chama tawala cha Waziri Mkuu Viktor Orban cha Fidesz.
Novak alikua mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa mkubwa wa urais wa Hungary tangu mwaka wa 2022.
No comments:
Post a Comment