NEWS

Monday 5 February 2024

Fedha za CSR Barrick North Mara zilivyopiga jeki ujenzi wa shule ya sekondari mpya kijijini Mrito



Upande wa mbele wa vyumba viwili vya madarasa vya Shule ya Sekondari Barata kijijini Mrito, ambavyo ujenzi wake umefadhiliwa na fedha za CSR Barrick North Mara.
--------------------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU
------------------------------------------


HISTORIA mpya imeandikwa. Ndivyo tunavyoweza kuelezea ujenzi wa shule ya sekondari mpya na ya kwanza katika kijiji cha Mrito kilichopo kata ya Kemambo wilayani Tarime, Mara.

Ujenzi wa shule hiyo ya sekondari ambayo imepewa jina la Barata, ulikamilika mwishoni mwa mwaka jana, na tayari imepokea wanafunzi 71 kati kati ya 84 waliotarajiwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwaka huu.

Kufunguliwa kwa shule hiyo ni sehemu ya matunda ya uwekezaji katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

“Tuliomba tukapewa shilingi milioni 141 kutoka vijiji sita kati ya 11 vinavyopokea fedha za CSR kutoka mgodi wa Barrick North Mara, ambazo zimetumika kugharimia ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na nyumba pacha ya walimu,” Diwani wa Kata ya Kemambo, Bogomba Rashid aliiambia Sauti ya Mara katani humo jana.


Diwani Bogomba Rashid
----------------------------------
Bogomba anavitaja vijiji hivyo sita vilivyoonesha ukarimu huo kuwa ni Kerende, Kewanja, Mjini Kati, Nyabichune, Nyangoto na Matongo vinavyopakana na mgodi wa North Mara uliopo Nyamongo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime [Vijijini].

Anasema ujio wa Shule ya Sekondari Barata umekuwa mkombozi kwa wanafunzi wanaoishi kijijini Mrito na baadhi kutoka vijiji jirani vya Msege na Gibaso.

Anafafanua kuwa kabla ya ujenzi wa shule hiyo, wanafunzi kutoka vijiji hivyo walikuwa wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 10 hadi 14 kwenda kusoma katika Shule ya Sekondari Kerende na kurudi nyumbani.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mrito, Chacha Irondo Ryoba na Mwenyekiti mstaafu, Edson Juma Mwita wanaishukuru Barrick North Mara wakisema, shule hiyo itaoondoa tatizo lililokuwepo la baadhi ya wanafunzi kuacha shule kutokana na adha ya kutembea umbali mrefu.


Chacha Irondo Ryoba
-------------------------------

Edson Juma Mwita
---------------------------
Shule ya Sekondari Barata sasa inafanya kata ya Kemambo kuwa na shule za sekondari tatu. Nyingine ni Kemambo na Ingwe.

“Waasisi wa shule hizi tatu ni wananchi, lakini hakuna shule ambayo mgodi wa North Mara haujaweka mkono,” anasema Diwani Bogomba anayetokana na chama tawala - CCM.

Bogomba anasema kata hiyo imelazimika kuwa na shule za sekondari tatu kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, kata ya Kemambo inayoundwa na vijiji vya Kewanja, Kerende na Mrito ina wakazi zaidi ya 29,098. Kati ya hao, wanaume ni 14,476 na wanawake ni 14,622.

Hata hivyo, diwani huyo anasema Shule mpya ya Sekondari Barata bado ina mahitaji mbalimbali kama vile jengo la utawala na nyumba nyingine za mwalimu.


Upande wa mbele wa nyumba pacha ya walimu katika shule mpya ya sekondari kijijini Mrito.
-------------------------------------------
“Nyumba ni motisha kwa walimu, na siyo vizuri kuwaacha waingie gharama kupa nyumba za kuishi. Hivyo tunaomba mgodi wa North Mara uendelee kutusaidia kwa sababu bado hii sekondari ya Mrito ina mahitaji mengi,” anasisitiza Bogomba.

Hivi karibuni, akiwa katika ziara ya kikazi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa alikwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa sekondari hiyo ya Mrito na kuagiza mamlaka husika kuhakikisha inakamilika haraka na kuanza kupokea wanafunzi mwaka huu.

“Naagiza hii shule ifunguliwe ili kuwapunguzia wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu, lakini pia kuepushia watoto wa kike vishawishi vinavyoweza kukatisha ndoto zao za elimu,” alisema Chandi.
Chanzo: SAUTI YA MARA
#tUkweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages