NEWS

Monday, 26 February 2024

Halmashauri ya Wilaya Bunda yaingia 18 za Waziri Mkuu, asema imekithiri kwa wizi na uzembe



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kulia), akizungumza wakati wa ziara yake 
wilayani Bunda leo.
------------------------------------------

Mwandishi wa Mara
Online News, Bunda
------------------------------


WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameikemea vikali Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, akisema imekithiri kwa wizi wa mali za umma na uzembe wa watumishi.

“Kila mahali ninapopita ni vilio tu Bunda, wiwi, wizi, wizi, wizi Bunda, hapa kuna uzembe mwingi, haturidhishwi na utendaji wenu, uaminifu ni mdogo… wizi ni mkubwa.

“Hapa saruji ilishaibwa, Bunda trend yenu ya uaminifu ni mdogo sana na mnafanya watumishi wa umma kutoaminika,” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa alipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi na kuweka jiwe la msingi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Mara, leo Februari 26, 2024.

“Halafu siyo hapa tu, hata hospitali ya wilaya ina matatizo mengi, mmeshang’oa milango, mmeshaiba vifaa vya ex-ray na kila kitu mling’oa, sit scan mling’oa,” ameongeza Majaliwa na kuhoji: “Ninyi Bunda mkoje? Kwanini Bunda wizi ni mkubwa?”

Mtendaji Mkuu huyo wa Serikali pia ameonesha kushangazwa na mamlaka husika kutochukua hatua za kisheria na kinidhamu dhidi ya watu wanaoendelea kuiba mali za umma katika halmashauri hiyo.

“Watu wanaiba kwa mara ya kwanza, mara ya pili. Ilitakiwa mchukue hatua za kuwadhibiti wasirudie tena mara ya pili, wizi umeshamiri, hatuwezi kwenda hivyo. DC (Mkuu wa Wilaya) dhibiti wizi huu, si hapa tu mpaka fedha za halmashauri, uzembe na wizi ni mwingi,” amesema Waziri Mkuu huyo.

Aidha, Majaliwa hakufurahia kutowakuta mafundi katika eneo la ujenzi wa shule hiyo - akitilia shaka hali hiyo kuwa huenda imetengenezwa kwa makusudi ili kujaribu kuficha ubadhirifu wa fedha za mradi huo.

“Miradi yote napokwenda watu wapo kazini, tunawasalimia, tunawauliza mnamaliza lini, watwambie kama fedha yao ipo. Mimi nimekuja kukagua kazi inavyoendelea, nilitakiwa niwaone leo. Sasa leo mmewaondoa wote ili wasiseme wizi na uzembe uliopo,” amesema.

Waziri Mkuu Majaliwa aliwasili mkoani Mara jana kwa ziara ya kikazi ya siku tano, ikiwemo kuzungumza na watumishi na viongozi, kufanya mikutano ya hadhara, kutembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za utawala, elimu, afya na miundombinu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages