NEWS

Wednesday 21 February 2024

Kamati ya Bunge yakagua miradi ya CSR Barrick North Mara



Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakikagua mradi wa kilimo biashara kijijini Matongo wakati wa ziara yao ya kikazi katika mgodi wa Barrick North Mara juzi.
-------------------------------------------

NA MWADISHI WETU, Nyamongo
--------------------------------------------------


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imekagua baadhi ya miradi ya kijamii iliyotekelezwa kutokana na fedha za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) zilizotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara uliyopo Nyamongo wilayani Tarime.

Miradi waliyotembelea wakati wa ziara yao ya kikazi katika mgodi wa North Mara juzi, ni nyumba za walimu, vyumba vya madarasa na maabara katika Shule ya Sekondari Matongo, mradi mkubwa wa majisafi Nyangoto na ule wa kilimo biashara ulioanzishwa kwa ajili ya kuwezesha vijana kiuchumi katika kijiji cha Matongo kinachopakana na mgodi huo.

Wabunge hao akiwemo Dkt Angeline Mabula aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, walieleza kufurahishwa na miradi hiyo na kuipongeza Kampuni ya Barrick Gold kwa kuwa chachu ya maendeleo ya jamii inayozunguka mgodi huo.

“Hii project ya maji ni kubwa, niwape (Barrick North Mara) big up kubwa,” alisema mmoja wa wabunge hao.


Tenki la mradi mkubwa wa majisafi Nyangoto
----------------------------------------
Naye Dkt Mabula alipongeza kampuni hiyo kwa kuendelea kuimarisha uhusiana na jamii inayozunguka mgodi huo.

Baadhi ya wabunge hao walisema walichokiona katika ziara yao hiyo siyo ambacho wamekuwa wakisikia.

Madiwani na wenyeviti wa serikali za vijiji 11 vinazunguka mgodi huo waliambia Kamati hiyo ya Bunge kuwa kwa sasa uhusiano kati ya mgodi huo na wakazi wa maeneo hayo ni mzuri, licha ya changamoto mbalimbali kama vile utwaaji wa ardhi pale mgodi unapohitaji kupanua shughuli zake.

Kamati hiyo pia ilielezwa kuridhishwa na shughuli za utunzaji wa mazingira katika mgodi huo.

“Mnatunza mazingira vizuri, wabunge wamefurahi - na kwa niaba yao ninawapongeza [Barrick North Mara], endeleeni kuwa watunzaji wazuri wa mazingira kwa usalama wa wananchi wetu,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, David Mathayo David.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages