NEWS

Tuesday 27 February 2024

Kero ya tembo waharibifu Mara yatua kwa Waziri Mkuu, wananchi waomba uzio kuikomeshaWaziri Mkuu, Kassim Majaliwa (juu ya gari), akizungumza na wananchi wilayani Bunda jana.
-------------------------------------

Na Mwandishi Wetu,
Mara Online News, Bunda
----------------------------------
-

WANANCHI wanaoishi jirani na Hifadhi ya Taifa Serengeti na mapori ya akiba ya Ikorongo- Grumeti upande wa wilaya ya Bunda mkoani Mara, wameiomba Serikali kuwasaidia kufanikisha hitaji lao la kujengewa uzio wa kuzuia tembo wanaovamia vijiji vyao na kuharibu mazao mashambani.

Waliwasilisha ombi hilo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliposimama kusalimia na kusikiliza kero za wananchi katika kijiji cha Mariwanda jana.

Walitaja uharibifu wa mazao ya chakula unaofanywa na tembo mara kwa mara kama kero kubwa inayowanyima maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa muda mrefu sasa.

Mwakilishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) alikiri mbele ya Waziri Mkuu kwamba kumekuwepo na ongezeko la migongano ya binadamu na wanyamapori wilayani Bunda.

Kuhusu uzio wa kuzuia tembo, mwakilishi huyo wa TAWA alisema suala hilo ni la kisera, hivyo litawasilishwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hatua za ufumbuzi.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali itaongeza nguvu ya kuzuia tembo waharibifu kuingia kwenye mashamba na makazi ya watu.

Kundi la tembo
----------------------
Tatizo la tembo kuvamia vijiji, kuharibu mazao na kutishia maisha ya wananchi linaonekana kukosa ufumbuzi kwa miongo kadhaa sasa, licha ya kuwepo juhudi zinazofanywa na taasisi za Serikali katika Wizara ya Maliasili na Utalii za kutafuta suluhisho la kudumu.

Wilaya ya Bunda ni miongoni mwa maeneo ya mkoa wa Mara yanayoathirika zaidi na tatizo la kuvamiwa na tembo wanaosababisha madhara makubwa.

Mbali na uharibifu wa mazao mashambani unaofanywa na tembo katika vijiji vinavyopakana na maeneo ya uhifadhi mkoani Mara, pia kumekuwepo na visa vya baadhi ya wananchi wa maeneo hayo kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Waziri Mkuu Majaliwa yupo mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ya siku tano ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo, kuhutubia mikutano ya hadhara na kusikiliza kero za wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages