NEWS

Tuesday 6 February 2024

Madiwani Tarime Vijijini wapitisha bilioni 9/- za CSR kutoka Barrick North Mara, Meneja Mahusiano awaomba kusaidia kutokomeza uvamizi mgodiniMwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo leo Februari 6, 2024. Waliokaa ni Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (kushoto) na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji, Solomon Shati.
-------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News, Tarime
------------------------------------


BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime [Vijijini], limepitisha mpango wa fedha za Uwajibikaji kwa Huduma za Kijamii (CRS) kutoka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Madiwani hao wamepitisha mpango huo katika kikao chao kilichofanyika Nyamwaga leo Februari 6, 2024 ambacho pia kimehudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la  Tarime Vijijini, Mwita Waitara, miongoni mwa viongozi wengine.


Madiwani kikaoni
-------------------------
Kiasi cha fedha za mpango huo kwa mwaka 2024 kilichopitishwa katika kikao hicho, ni shilingi bilioni tisa kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii, huku ununuzi wa madawati ya shule za msingi na sekondari ukipewa kipaumbele.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simion Kiles ameweka wazi kuwa asilimia 60 fedha hizo imeelekezwa kwenye vijiji 77 na asilimia 40 imekwenda kwenye vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi wa North Mara.

“Kati ya asilimia 60 iliyoelekezwa kwenye vijiji 77, asilimia 30 imeelekezwa kwenye miradi ya kimkakati ya halmashauri na 30 imeenda kwenye vijiji husika,” amefafanua Kiles ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakonga kwa tiketi ya chama tawala - CCM.Akizungumzia suala la madawati, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Solomon Shati amesema shule za msingi zina uhitaji wa madawati 11,000 na uhitaji kwenye shule za sekondari ni madawati 8,000.

Kwa mujibu wa Shati, ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya CSR ndani ya halmashauri hiyo umeendelea kuongezeka siku hadi siku.


Solomon Shati
-----------------------
“Tumezidi kuboresha utekelezaji wa miradi ya CSR, ukichukua miradi ya mwaka 2019/2020 wakati CSR inaanza, ukailinganisha na miradi ya CSR kipindi hiki ni vitu viwili tofauti, na tumeendelea kushirikiana na wenzetu wa mgodi vizuri,” alisema Shati.

Kwa upande wake, Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi ametumia nafasi hiyo kuwaomba madiwani hao kusemea miradi ya CSR katika kata zao, pamoja na kusaidia kukemea vitendo vya uvamizi mgodini vinavyofanywa na makundi ya watu wanaojulikama kama ‘intruders.


Meneja Uhadi akizungumza kikaoni
--------------------------------------------
“Mpaka sasa bado uvamizi wa mgodi ni tatizo kubwa sana, kwa hiyo niwaombe kwa upande wenu [madiwani] mlichukulie suala hili kwa uzito. Tunaamini kwamba uzalishaji utaenda vizuri na tutapata fedha za CSR nyingi zaidi pale ambapo mgodi unafanya kazi katika hali ya utulivu.

“Pia, tunawaomba mkatangaze kwenye kata zenu kwamba miradi hiyo inayotekelezwa chini ya CSR imetoka mgodini, maana kuna watu wengine wanafikiri mgodi hautoi fedha kwenye jamii kwa sababu hawana taarifa sahihi,” amesema Uhadi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages