NEWS

Thursday 8 February 2024

Prof Muhongo ashauri mabadiliko makini katika mfumo wa elimu, ataka mitihani iachane na maswali ya kuchagua.


Na Mwandishi wa
Mara Online News, Dodoma
------------------------------------

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo ameitaka serikali kufanya mageuzi makubwa katika mfumo wa elimu ikiwa ni pamoja na kuachana na maswali ya kuchagua ili kuwajengea wanafunzi na wahitimu umahiri unaotakiwa katika soko la ajira kimataifa.

Akichangia bungeni jana, Prof Muhongo alisema mfumo uliopo wa kutahini wanafunzi kuanzia ngazi za chini hadi Chuo Kikuu hauwezi kuwasaidia wanafunzi kupata maarifa stahiki na ujuzi kwenye maeneo wanayosomea.

Alisema mitaala lazima iwasaidie wanafunzi kuwa wadadisi na kuwa wabunifu na akaonesha kushangazwa na mtindo unaojitokeza kwa kasi siku hizi wa watu kulipa fedha ili kufanyiwa tafiti na kuandaliwa andiko la utafiti husika kabla ya kutunukiwa shahada ya Chuo Kikuu.

"Sasa hivi kuna watu wanalipwa fedha ili kuwafanyia wasomi tafiti na kuandikiwa paper hii huwezi kuikuta nchi nyingine. Iko Tanzania tu," amesema.

Mbunge huyo kutoka chama tawalawa -CCM ameitaka pia serikali kufanya maboresho makubwa ya Tume ya Sayansi na Technologia (COSTECH) na kuiwezesha iondoke katika mfumo wake wa sasa ili kuweza kusimamia vema mageuzi makubwa ya kisayansi na kiteknolojia nchini.

Kwa mujibu wa Profesa Muhongo Tanzania inatakiwa kuchangamkia soko kubwa la ajira katika maeneo makubwa sita ambayo wataalam wake wanatafutwa sana dunia nzima.

Ameyataja maeneo hayo kama utaalam wa mifumo ya kompyuta (software developers,) utaalam wa data (data science), uchambuzi wa usalama wa taarifa mtandao (information security analyst), usimamizi wa mifumo (management analyst), utaalam wa technolojia ya akili bandia (artificial intelligence specialist) na wauguzi kwenye maeneo mbali mbali ya kitaalam (practicing nurses)

Alisema wauguzi wanahitaka sana hasa baada ya wimbi la ugonjwa wa korona lililoangamiza wataalam wengi wa afya wakiwemo wauguzi na madaktari.

Professor Muhongo alisema uchumi wa dunia unakuwa kwa kasi kubwa akitoa mfano wa Mwaka jana 2023 ambapo uchumi wa dunia ulikuwa na thamani ya dola za kimarekani trillion 105 huku maeneo hayo sita ya kitaalam yakiongoza kwa kuchangia uchumi huo.

Alitoa mfano wa nchi ya India ambayo uchumi wake unapaa kwa kasi kutoka na kuwekeza sana katika nyanja za kiteknolojia hasa teknologia ya Blockchain, biashara ya kidigitali, sayansi ya data na akili bandia.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages