NEWS

Thursday 29 February 2024

Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi “Mzee wa Ruksa’ aaga dunia kwa saratani ya mapafu, Rais Samia atangaza siku 7 za maombolezo ya kitaifa



Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi enzi za uhai.
-----------------------------------------


Na Mwandishi Wetu
---------------------------

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 98.

Ali Hassan Mwinyi alizaliwa Mei 5, 1925 na aliongoza Serikali ya Awamu ya Pili Tanzania baada ya kuingia madarakani rasmi Novemba 5, 1985.

Rais wa Awamu ya Sita Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan alilitangazia Taifa kuwa Mwinyi alifariki dunia jana Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikopokuwa akiendelea kupatiwa matibabu ya ugonjwa wa saratani ya mapafu.

“Hayati mzee Ali Hassan Mwinyi, amekua akipatiwa matibabu tangu Novemba mwaka jana nchini Uingereza, na baadaye kurejea nchini alipokuwa akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Mzena, hadi umauti ulipomfika,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Rais Samia alitangaza kuwa Tanzania itaombeleza msiba huo wa kitaifa kwa siku saba kuanzia leo Machi 1, 2024 huku bendera zikipepea nusu mlingoti.

Rais huyo wa zamani anatarajiwa kuzikwa kesho Machi 2, 2024 visiwani Zanzibar.

Katika safari yake ya kisiasa, Ali Hassan Mwinyi alijiunga na Chama cha Afro Shiraz (ASP) mwaka 1964 na kushika nyadhifa mbalimbali za Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aliwahi kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Zanzibar mwaka 1963, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1970 na kati ya mwaka 1982 hadi 1983 alikuwa Waziri wa Afya.

Pia aliwahi kuwa Waziri Mambo ya Ndani, Maliasili na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri.

Mwaka 1984 alichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwaka 1985 alichaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Pili ya Serikali ya Muungano wa Tanzania hadi mwaka 1990 alipochaguliwa tenda kwa muhula mwingine hadi mwaka 1995 alipostaafu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages