
Waziri Bashiru akizungumza na wananchi wilayani Butiama, Agosti 12, 2026. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi.
Butiama
--------------
Wananchi wa mkoa wa Mara wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuenzi na kulinda tunu za taifa alizoziacha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambazo alizipigania kikamilifu katika uhai wake.
Tunu hizo ambazo zimelishikilia kwa pamoja taifa la Tanzania ni amani, uzalendo, undugu na mshikamano usiotikisika.
Wito huo ulitolewa Agosti 12, 2026 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt Bashiru Ally Kakurwa, ambaye alikuwa na ziara ya siku nne ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo mkoani Mara.
“Wito wangu kwa wana-Mara ni ninyi kuwa mfano katika taifa letu kwa kudumisha amani, uzalendo, undugu, umoja na mshikamamno wa kitafa,” alisema Waziri Bashiru wakati akihutubia mkutano wa hadhara.
Alisisitiza umuhimu wananchi wa mkoa huo na Watanzania kwa ujumla kuendelea kulinda amani na utulivu kwa ustawi wa taifa.
Alisema wilaya ya Butiama imebeba historia ya uongozi wa nchi ya Tanzania kutokana na mambo mazuri aliyoyafanya Mwalimu Nyerere katika kujenga uongozi imara nchini.
“Mwalmu Nyerere alifanya kazi kubwa kwa kutuunganisha na kuwa taifa imara lenye mshikamano,” alisema Waziri Bashiru, ambaye katika ziara hiyo alifuatana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi.
Aidha, aliwaomba wananchi wa mkoa huo kuendelea kuiunga mkono serikali ili kuleta kasi ya maendeleo nchini.
“Tumuunge mkono Rais wetu [Dkt. Samia Suluhu Hassan] anayeendeleza maono ya Baba wa Taifa kwa kuwekeza kwenye elimu kwa kujenga vyuo hapa,” alisema Waziri Bashiru.
Serikali ya Awamu ya Sita tayari imewekeza mabilioni ya fedha katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Juluius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia wilayani Butiama.
No comments:
Post a Comment