NEWS

Saturday 10 February 2024

Mazungumzo ya Rais Samia na Rais Duda wa Poland yalivyozibeba sekta nyetiRais Samia Suluhu Hassan na Rais Andrzej Duda wa Poland wakiwa katika mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
---------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
----------------------------


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Poland, Andrzej Duda, wamekubaliana nchi hizo ziendeleze ushirikiano zaidi katika uboreshaji wa sekta mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili.

“Tumekubaliana kuendelea kushirikiana zaidi katika maeneo ya elimu, kilimo, biashara, uwekezaji, utalii na TEHAMA eneo ambalo wenzetu wamepiga hatua kubwa,” aliandika Rais Samia katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii, baada ya kufanya mazungumzo na Rais Duda, Ikulu jijini Dar es Salaam jana.

“Kiuchumi, tumeweka nia ya pamoja na kuazimia kuhamasisha uwekezaji zaidi kwenye sekta za kimkakati kama viwanda, uzalishaji, nishati, madini, gesi asilia na uchumi wa bluu,” alisema.


Rais Samia na Rais Duda wakiwa wamesimama kwa ukakamavu wakati Wimbo wa Taifa ukiimbwa katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
-----------------------------------------
Rais Samia alisema Poland ni nchi ya 21 kwa ukubwa wa kiuchumi duniani na mshirika muhimu wa Tanzania katika Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU).

Alisema Tanzania na Poland zinashirikiana katika maeneo mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wa mataifa hayo, hasa kwenye utalii ambapo Poland ni kati ya nchi 10 zinazoleta watalii wengi zaidi nchini.

“Kutokana na ukuaji huu wa biashara ya utalii baina yetu, nimemueleza nia yetu ya kuwa na safari za moja kwa moja za ndege kutoka Poland kuja Tanzania.

“Mbali na utalii, pia tuna ushirikiano mkubwa katika sekta ya afya, wakishiriki nasi miradi kwenye hospitali za Aga Khan, Temeke, Mwananyamala, Kituo cha Afya Chanika na Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana.

“Nimeshukuru pia kwa utayari wa nchi yake kupitia wakala wa mikopo ya usafirishaji kutoa bima kwa benki za biashara katika utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa nchini kwa vipande vya Makutopora - Tabora na Tabora - Isaka.

“Kwa ujumla, sote tumeona kwamba kwa umri na historia ya ushirikiano uliopo kati yetu [Tanzania na Poland], masuala ya biashara na kuinua uchumi bado ni madogo, hivyo basi lazima kuongeza ushirikiano wetu kiuchumi kwa njia za uwazi, haki na kuaminiana.

“Mheshimiwa Rais [Duda] amenipa pia mwaliko wa kutembelea Jamhuri ya Poland, na mimi nimemuahidi kuwa panapo majaliwa, mimi na ujumbe wangu kwa niaba ya nchi yetu tutafanya ziara ya kitaifa nchini humo,” alisema Rais Samia.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages