NEWS

Monday 19 February 2024

Serikali yaja na suluhisho la changamoto ya nishati ya umeme migodini




Na Mwandishi Wetu, Dodoma
----------------------------------------


SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imeanza mazungumzo na Kampuni ya TAQA-DALBIT kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa upatikanaji wa nishati ya umeme migodini na maeneo yenye wachimbaji wadogo, ili kuchochea shughuli za uchimbaji madini nchini.

Mazungumzo hayo yalifanyika jijini Dodoma juzi - yakiongozwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akisaidiana na Naibu Waziri Madini, Dkt Steven Kiruswa na Menejimenti ya Uongozi wa Kampuni ya TAQA-DALBIT iliyoongozwa na Meneja Mkuu, Amr Aboushad na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara, Raphael Banzi.

Akiwasilisha maelezo ya awali, Aboushad alisema kampuni yao ipo tayari kuja na mpango wa uzalishaji wa umeme kupitia gesi kwa kufunga mitambo katika migodi na maeneo ya wachimbaji - itakayosaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa zaidi ya nusu ya gharama inayotumika kwa sasa kupitia matumizi ya mafuta ya dizeli na petroli.

Alisema awamu ya pili itahusisha uzalishaji wa umeme kupitia mfumo wa umeme jua ambapo kampuni hiyo itafunga mtambo mkubwa kwa gharama yao na kuwaunganisha wachimbaji wadogo kwa malipo ya mwezi kwa matumizi ya nishati hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Madini, Mavunde, aliishukuru Kampuni ya TAQA-DALBIT kutoka Falme za Kiarabu (UAE) yenye ofisi zake nchini Tanzania, kwa utayari wa kutatua changamoto ya upatikanaji wa nishati ya umeme migodini na kuagiza uongozi wa wizara kuitisha mkutano wa haraka na wadau wote, wakiwemo wachimbaji wadogo na wakubwa ili kupata fursa ya kujadiliana namna bora ya utekelezaji wa mpango huo.

"Utekelezaji wa mpango huu utasaidia sana kuchochea shughuli za uchimbaji nchini Tanzania na hivyo kuongeza uzalishaji wa madini," Waziri Mavunde alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages