NEWS

Friday 16 February 2024

Walimu Sekondari ya Kenyamanyori wapewa motisha kwa matokeo mazuri kidato cha nne 2023
Na Godfrey Marwa, Tarime
-------------------------------------


UONGOZI wa Shule ya Sekondari ya Kata Kenyamanyori wilayani Tarime, Mara umewazawadia walimu wa shule hiyo fedha taslimu, kuonesha kutambua na kuthamini juhudi zao za kufundisha - zilizowezesha wanafunzi wao kufanya vizuri katika mtihani wa taifa wa kuhitimu kidato cha nne mwaka 2023.

Hafla ya kukabidhi zawadi hizo ilifanyika shuleni hapo jana, ikiongozwa na Mkuu wa Shule hiyo, Mwl Chacha Lukas Nyaite, ambapo aliyewakabidhi ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Novertus Kibaji, mbele ya viongozi wengine na wananchi mbalimbali.Mwl Nyaite alisema uongozi wa shule hiyo umetoa zawadi hizo kuwamotisha walimu kuendelea kujituma katika kufundisha ili kuwezesha wanafunzi wao kufanya vizuri zaidi katika mitihani ya kitaifa.Kwa mujibu wa Mwl Nyaite, shule hiyo ambayo ni ya wanafunzi mchanganyiko [wavulana na wasichana], imeweza kufanya vizuri kwa miaka mitatu mfululizo katika mitihani ya taifa ya kuhitimu kidato cha nne, ambapo kwa matokeo ya mwaka 2023 imefanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika Halmashauri ya Mji wa Tarime na nafasi ya tatu kimkoa.

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa katika matokeo ya mwaka 2023, wanafunzi wote 86 walifaulu, ambapo 13 walipata daraja la kwanza, 14 daraja la pili, 19 daraja la tatu na 40 daraja la nne.Hafla hiyo ya kukabidhi zawadi kwa walimu ilifuatiwa na harambee ndogo ya kuchangia ujenzi wa bweni/ hosteli kwa ajili ya wanafunzi wa kike shuleni hapo.

Habari za kina kuhusu harambee hiyo zitachapishwa kwenye toleo lijalo la Gazeti la Sauti ya Mara - ambalo ni chombo dada cha Blogu ya Mara Online News.


Mkuu wa Shule ya Sekondari Kenyamanyori, Mwl Chacha Lucas Nyaite akizungumza katika hafla hiyo jana,
--------------------------------------------

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages