NEWS

Thursday 29 February 2024

Waliomzomea Mbunge Esther Matiko waitwa ‘genge hatari’, wachambuzi wa siasa wamtabiria makubwaMbunge Esther Matiko
-------------------------------

NA MWANDISHI WATU, Tarime
----------------------------------------------


WANANCHI mbalimbali wamelaani kitendo kilichofanywa na kundi la watu waliomzomea Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Esther Matiko alipopewa na nafasi kuzungumza katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa mjini Tarime juzi.

Wameliita kundi hilo kuwa ni ‘genge hatari’ na lisilojua maana ya maendeleo.

“Mheshimiwa Esther alikuwa anazungumzia maendeleo ya Tarime Mjini na alikuwa na ‘point’ zenye mashiko, hakupaswa kuzomewa na hili genge,” alisema mmoja wa wakazi wa Tarime Mjini.

Baadhi ya wananchi wakiwemo makada wa chama tawala -CCM, mbali na kulaani kitendo hicho walionesha kufurahiswa na hoja alizozitoa Esther katika mkutano huo.

“Tunalaani kitendo cha kumzomea Esther kwa sababu alikuwa anazungumzia maslahi ya wilaya na mkoa wetu, mfano alisema Shule ya Sekondari Mogabiri iwe na kidato cha tano na cha sita, na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu alielekeza Halmashauri waandike barua kuomba iwe High school,” alisema mkazi mwingine wa Tarime.

Inaelezwa kuwa kundi liliofanya zomeazomea hiyo liliratibiwa na kigogo mmoja (tunahifadhi jina lake kwa sababu bado hatujazungumza naye) kutokana na hofu ya kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2025.

“Kitendo cha kumzomea Mheshimiwa Esther Matiko akiwa anawasilisha hoja za kimaendeleo mbele ya Waziri Mkuu kimeitia aibu Tarime,” alisema kada na kiongozi wa CCM wilayani humo ambaye hakupenda kutajwa jina.

Sauti ya Mara ilipomuuliza Mbunge Esther kuhusu suala hilo alisema yupo imara na hakutetereka na kilichojaribu kukatisha mazungumzo yake mbele ya Waziri Mkuu.

“I am not disappointed, nipo strong zaidi, na kilichofanyika kimegeuka kuwa positive (Chanya) kwangu,” Esther ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini mwaka 2015-2020 aliliambia Gazeti la Sauti ya Mara kwa njia ya simu jana.

Hata hivyo, wachambuzi wa msuala ya siasa wilayani Tarime wameeleza kuwa kitendo hicho kinaweza kumuinua zaidi mwanasiasa huyo na kugeuka pigo kwa walioratibu mpango huo wa kumzomea.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages