Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akipata maelezo ya mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma kutoka kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe (kulia) jana.
---------------------------------------
-------------------------------------------
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amefurahishwa na uwezo wa uthubutu na ubunifu wa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe katika ujenzi wa barabara za lami mkoani humo.
Majaliwa alionesha furaha hiyo akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Rorya juzi, baada ya Meneja huyo wa TANROADS kumweleza jinsi ofisi yake ilivyojipanga kujenga barabara ya Kuruya-Kinesi kwa kiwango cha lami.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, barabara ya kutoka Kuruya mpaka Kinesi Bandarini ni ya TANROADS na ina urefu wa kilomita 18.42. Tulikuwa tunapewa hela kidogo kidogo kuijenga kwa kiwango cha lami, tumeanzia pale Kuruya mita 100 lakini kwa jinsi urefu wa barabara ulivyo tukijenga mita 100 kila mwaka tutahitaji miaka 180 kuikamilisha.
“Lakini kama TANROADS tukajiongeza tukasema hiyo haiwezekani wananchi wa Kinesi wanahitaji barabara ya lami kwa ujumla, tukaomba fedha Serikali ya Mama Samia [Rais Dkt Samia Suluhu Hassan] imetuletea shilingi milioni 184 tumeanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu kwa ajili ya kuijenga yote kwa kiwango cha lami.
“Kwa hiyo mwezi wanne [akimaanisha Aprili 2024] tunategemea usanifu utakamilika na ukikamilika tutakuwa tunajua makisio ya kuijenga ile barabara, tutaomba fedha tutaanza kuijenga mara moja,” Mhandisi Maribe alimweleza Waziri Mkuu.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe akimweleza Waziri Mkuu jinsi ofisi yake ilivyojipanga kujenga barabara ya Kuruya-Kinesi Bandarini.
---------------------------------------
Baada ya maelezo hayo Waziri Mkuu Majaliwa alimpongeza Meneja huyo wa TANROADS Mkoa wa Mara kwa uamuzi aliofanya kuelekea ujenzi wa barabara hiyo ya Kuruya-Kinesi Bandarini kwa kiwango cha lami.
“Asante sana Injinia (Mhandisi), mmefanya vizuri sana kuiangalia barabara hiyo. Nimefurahi kusikia kwamba TANROADS hapa mkoani wamejiongeza kwa kuona umuhimu wa barabara hii ya Kuruya mpaka Kinesi Bandarini, huko ni kujiongeza - mpigieni makofi Meneja wa TANROADS.
“Kwa hiyo Meneja wa TANROADS hongera kwa kuiona hii barabara kwamba ina umuhimu wake inaenda bandarini eneo la uvuvi, hongera sana Meneja wa TANROADS mnaendelea vizuri,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa na kuitaka Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kuiunga mkono ofisi ya Mhandisi Maribe katika jitihada za ujenzi wa barabara hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu huyo, TANROADS ilianza na ujenzi wa barabara za kuunganisha mikoa na zile za mipaka ya Tanzania na mataifa mengine lakini kwa sasa inatekeleza mkakati wa kiserikali wa kujenga barabara zinazounganisha wilaya na wilaya nchini.
“Tuko kwenye mipango ya kuunganisha wilaya na wilaya, ndiyo sababu sasa tunajenga barabara ya lami kutoka Butiama inapitia Bunda inakuja Mugumu wilaya ya Serengeti, na tunajenga barabara kutoka Serengeti kuja Tarime na wakandarasi wako kazini kwa mkoa huu. Baadaye tutaanza kuiangalia barabara inayotoka hapa [Rorya] mpaka Serengeti moja kwa moja baada ya kuwa tumemaliza barabara kutoka Makutano mpaka Butiama,” alisema Majaliwa.
Barabara zinazojengwa
Awali, wakiwa wilayani Serengeti, Mhandisi Maribe alitaja mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa barabara za lami zinazojengwa kwa sasa mkoani Mara kuwa ni Makutano-Sanzate, Natta-Mugumu inayounganika na ya Mugumu-Tarime.
Meneja huyo wa TANROADS Mkoa wa Mara alisema tayari barabara ya Makutano-Sanzate yenye urefu wa kilomita 50 imekamilika kwa asilimia 100.
“Kuanzia Sanzate hadi Natta (kilomita 40) bado inaendelea, mkandarasi yuko site (kazini) na ujenzi wake umefikia asilimia 44. Tunategemea mwishoni mwa mwaka huu watakuwa wamemaliza hiyo kazi. Tunaendelea kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha anamaliza hiyo kazi,” Mhandisi Maribe alimweleza Waziri Mkuu Majaliwa.
Aliendelea: “Lakini pia, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania [Dkt Samia Suluhu Hassan] ametoa fedha kwa ajili ya kujenga barabara ya lami kilomita 87.14 kutoka Tarime mpaka Mugumu na sasa hivi kazi imeanza awamu ya kwanza kutoka Mogabiri mpaka Nyamongo kilomita 25 mkandarasi yuko site, na kutoka Nyamongo mpaka Mugumu mkandarasi pia yuko site.”
Waziri Mkuu Majaliwa alikubaliana na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Esther Matiko kwamba mkoa huo una hitaji kubwa la kuimarishiwa barabara zinazunganisha wilaya zake na mikoa jirani.
Waziri Mkuu Majaliwa akizungumzia barabara hizo.
--------------------------------------
“Ni kweli tuna barabara nyingi, na barabara hizi zinahitaji kuimarishwa. Barabara ya Sanzate-Natta, lakini pia Mugumu-Mto wa Mbu (Arusha), Mugumu-Butiama, Mugumu-Tarime; hizi ni barabara ambazo tayari wakandarasi wameshapewa.
“Iliradi wakandarasi wapo wameshapewa kazi, Meneja wa TANROADS sasa wasimamie, kila mkandarasi asimamiwe. Tulipopita pale Issenye umewasikia pia wananchi wakionesha mkandarasi anafanya kazi polepole, fuatilia kwa karibu ili hawa wamalize kazi hizi kwa wakati na wananchi wanatamani kuzitumia barabara hizo,” alisisitiza Mtendaji Mkuu huyo wa Serikali.
Aliongeza kuwa uchumi wa wilaya ya Serengeti na mkoa wa Mara kwa ujumla unategemea mawasiliano ya barabara, hasa za lami ili kuwezesha watu kuingia na kufanya biashara na kutoka kirahisi.
“Barabara hizi hapa kwetu ni fursa ya kila mmoja kujishughulisha kwenye eneo ambalo anahitaji kujishughulisha. Mheshimiwa Mbunge [Esther Matiko] amezungumzia pia barabara za mijini na zile ambazo zinakatika, zile siyo za TANROADS ni za TARURA (Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania),” alisema Waziri Mkuu Majaliwa na kumtaka Meneja husika kuzitolea maelezo.
Kwa mujibu wa msemaji wa TARURA mkoani Mara, barabara hizo ziko kwenye mpango wa bajeti ya mwaka 2023/24 na 2024/25, na kwamba kwa sasa miradi miwili iliyopo kwenye bajeti ya mwaka 2023/24 inaendelea kutekelezwa, huku mingine kadhaa ikiwa kwenye hatua za manunuzi.
Baada ya kupata majibu hayo, Waziri Mkuu Majaliwa aliitaka TARURA kuanza kutandaza lami kwenye barabara muhimu, hata kwa kutumia mapato ya ndani badala ya kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu pekee.
“Tunategemea mno fedha kutoka Serikali Kuu tu, Serikali Kuu tunafanya mambo mengi kwenye halmashauri. Fedha za ndani tunazokusanya zifanye kazi zinazoonekana,” alisema Majaliwa na kuhitimisha kwa kuwataka wakurugenzi na madiwanni kuiunga mkono Serikali Kuu kwa kutumia mapato ya ndani kugharimia uboreshaji wa barabara za mijini.
Uwanja wa Ndege Musoma
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amekagua mradi wa upanuzi na maboresho ya Uwanja wa Ndege Musoma unaotekelezwa chini ya usimamizi wa TANROADS Mkoa wa Mara.
Mhandisi Maribe alimweleza Waziri Mkuu kuwa mradi huo wenye thamani ya shilingi zaidi ya bilioni 35 unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 na kwamba utekelezaji wake ufikia asilimia 55.
Waziri Mkuu Majaliwa alipongeza hatua hiyo akisema uwanja huo utafungua fursa za kiuchumi na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii mkoani Mara, vitu ambavyo havikuwepo kutokana na kukosekana kwa uwanja wa ndege unaokidhi mahitaji ya watalii.
“Uwanja huu sasa utaleta fursa kwa wananchi wa mkoa huu na wilaya zake - sababu tumeipoteza fursa moja muhimu sana na kwa miaka mingi - ya kuleta watalii moja kwa moja kwenye mkoa huu na kwenda Serengeti [Hifadhi ya Taifa Serengeti].
“Leo Serengeti inatamkwa inaambatanishwa na mkoa wa Arusha na ilitakiwa Serengeti [Hifadhi] itamkwe na mkoa wa Mara na wilaya ya Serengeti. Lakini tatizo lilikuwa ni mahali pa kutua (uwanja wa ndege).
“Serikali inapojenga uwanja huu wana-Mara pamoja na uongozi wa mkoa ni lazima tufanye kazi moja kubwa sana ya kuutangaza kuanzia sasa uwanja huu unapokwenda kukamilika, lazima dunia ijue kwamba Serengeti [Hifadhi] ni ya mkoa wa Mara.
“Kukamilika kwa uwanja huu tunaamini sasa fursa ziwe kwa wananchi wa hapa lakini pia mikoa jirani, nchi jirani. Tutautumia sana uwanja huu, na kampeni hii iende sambamba na uwekezaji unaolenga kuvuta watalii wengi.
“Huu ni wakati sasa wa fursa kwa wana-Musoma, wana-Mara na mwingine yeyote mwenye uwezo wa kujenag hoteli ya nyota nne, tano na kuendelea. Tunahitaji hoteli, tunahitaji maeneo ya huduma na vijana wetu wahamasishwe kushiriki katika biashara za kuvutia watalii,” alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Kiongozi huyo wa kitaifa alihitimisha ziara yake ya siku tano mkoani Mara jana Alhamisi, ambapo katika ziara hiyo, alipata fursa ya kuzungumza na viongozi, kukagua, kuzindua, kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo, kuhutubia mikutano ya hadhara, kusikiliza kero za wananchi na kuzitolea maagizo ya ufumbuzi.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment