NEWS

Friday 15 March 2024

AICT, Right to Play waitaka jamii kutoa taarifa za watoto wa kike wanaoishi mazingira magumu



Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo akitoa wito kwa jamii kutoa taarifa za watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu, wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi katika Shule ya Msingi Nyansincha leo Machi 15, 2024.
----------------------------------------------

Na Josesh Maunya, Tarime
------------------------------------


KANISA la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Right to Play, limeitaka jamii kutoa taarifa za uwepo wa watoto wa kike wanaoshindwa kuendelea na masomo yao kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwamo hali ngumu ya maisha ili wapatiwe msaada na shirika hilo.

Hayo yamesemwa leo Machi 15, 2024 na Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo, wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi la uhamasishaji kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, lililoandaliwa na Right to Play kwa ushirikiano na AICT katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyansincha iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara.


Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyansincha wakifurahia kuonesha makombe ya ushindi.
--------------------------------------------

"Kama kuna mtoto wa kike hajapelekwa shule basi apelekwe apate elimu, lakini pia kama ana mazingira magumu mnaweza mkatoa taarifa kwa walimu na viongozi wengine ambao watatupa taarifa kwamba kuna binti ambaye hana uwezo wa kufika shuleni na shirika litafanya sehemu yake ili huyo binti apate elimu iliyo bora," amesema Fungo.

Kwa upande wake Diwani Kata ya Nyansincha, Samwel Chacha Muhono amelishukuru Right to Play kwa kufanya matamasha ya michezo ya kiuhamasishaji katika kata yake kwani yamekua na faida nyingi, ikiwemo elimu inayotolewa kupitia ujumbe unaoenezwa na shirika hilo.

"Niwashukuru sana wenzetu wa Right to Play kwa kuendelea kuleta matamasha haya katika kata yetu, na hii isiwe mara ya mwisho, bali muendelee kuja mara kwa mara, maana licha ya hii elimu mnayotupatia lakini pia tunapata faida zingine, mfano kupitia hili tamasha sisi viongozi tunapata fursa ya kukutana na wananchi, lakini pia michezo inaibua vipaji na kijenga afya za watoto wetu," amesema Diwani Muhono.


Diwani Muhono (katikati) na Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyansincha, Mwita Mwera wakikabidhi kwa mwakilishi wa washindi katika tamasha hilo.
----------------------------------------------

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyansincha, Hamis Ikila Ramadhan amesema matamasha hayo yanayoandaliwa na AICT pamoja na Right to Play pia yanasaidia kupunguza utoro kwani yanavutia na kuhamasisha wanafunzi kuhudhuria shule kwa wingi na kupenda masomo.

"Watoto wa kike wasaidiwe wasome kwa bidii kwa sababu kukatishwa masomo kunaleta athari mbalimbali kama umaskini, hivyo naiomba Serikali ichukue hatua kwa wazazi wanaowakatisha masomo watoto wa kike," amesema Jackline Samson, mwanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo.

AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe pia wamekuwa wakishirikaiana na Right to Play kuendesha mradi wa kukuza elimu iliyo bora na jumuishi kwa kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi kupitia matamasha ya michezo na midahalo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages