NEWS

Friday 29 March 2024

Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini haina ‘mortuary’ kwa miaka minne sasa
NA MWANDISHI WETU, Tarime
----------------------------------------------


WANANCHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) wanalazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kuhifadhi miili ya wapendwa wao, kutokana na ukosefu wa chumba cha kuhifadhi maiti (mortuary) kwa miaka zaidi ya minne katika Hospitali ya Halmashauri hiyo ambayo ujenzi wake unaripotiwa kugharimu mamilioni ya fedha.

Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida, kibao kilichopo kinaonesha kuwa mortuary ni miongoni mwa huduma zinapatikana hospitalini hapo, ilhali ukweli ni kwamba huduma hiyo haipo tangu hospitali hiyo ianze mwaka 2019.

“Katika ukanda huu wa Tarime Vijijini hakuna huduma za mortuary hadi uende katika kituo cha afya Sisrari, hapa kwetu hatuna hudumza hizo,” alisema mtumishi wa halmashauri hiyo kwa sharti la kutotajwa jina.

Baadhi ya vijiji ambavyo wakazi wake wanalazimika kusafiri umbari mrefu kutafuta huduma za mortuary ni Gibaso na Kegonga vilizopo jirani na Hifadhi ya Taifa Serengeti. vijiji hivyo vipo katika kata za Nyanungu na Kwihancha.

Wakizungumza na Sauti ya Mara kwa nyakati tofauti hivi karibuni, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nyamwaga ilipo hospitali hiyo, walisema ukosefu wa huduma za mortuary umekuwa kero kubwa nay a muda mrefu kwao.

“Hospitali hii kukosa huduma ya mortuary ni uzembe, hii ni halmshauri yenye mapato yakiwemo mabilioni ya fedha kutoka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, ni aibu kuona wananchi wanaendelea kutaabika kutafuta huduma hiyo maeneo ya mbali,” alisema alisema Ambrose Chacha.

Kwa mujibu wa Ambrose, baadhi ya wananchi wenye kipato cha chini wanalazimika kuzika wapendwa wao bila kufanya maandalizi kutokana na ukosefu huduma za mortuary hospitalini hapo.

“Wananchi wasiokuwa na uwezo wa kifedha wanawahi kuzika wapendwa wao bila ndugu waishio mbali kufika kushiriki, hii ni aibu kubwa,” aliongeza Amabrose ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyamwaga.

Taarifa zinasema baadhi ya wananchi wanalazimika pia kusafirisha miili ya ndugu, jamaa na rafiki zao kwenda kuihifadhi kwenye vituo vya afya vilivyo mbali na hospitali hiyo.

“Tunaomba Serikali itujengee mortury hapa [Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime - Vijijini] ili kutupunguzia gharama za kusafiri kwenda mjini Tarime na Sirari kutafuta huduma za kuhifadhi miili ya ndugu zetu maana hata kama una uwezo wa kifedha bado ni usumbufu,” alisema mkazi mwingine wa kijiji hicho aliyejitambuisha kwa jina la Jackline Mwita.

Diwani wa Kata ya Nyamwaga, Mwita Marwa aliidokeza Sauti ya Mara kuwa kwa sasa ujenzi wa mortuary katika Halmashauri hiyo umetengewa shilingi milioni 900.

“Hospitali yetu ya Halmashauri ya Wilaya tayari imetengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mortuary katika bajeti ya mwaka 2023/2024,” alisema diwani huyo anayetokana na chama tawala - CCM.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Solomoni Shati alipoulizwa na Sauti ya Mara kuhusu tatizo hilo la ukosefu wa mortuary alijibu kwa kifupi: “Sijapata hayo malalamiko lakini tunaendelea, tuko kwenye bajeti yake.”
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages