NEWS

Monday 11 March 2024

Kampuni 19 zahitimu mafunzo ya biashara Barrick North MaraBaadhi ya wamiliki na wafanyakazi kampuni 19 zilizohitimu mafunzo ya biashara wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka (katikati mwenye koti jeusi) na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko (kushoto kwa Chikoka).
------------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu, Nyamongo
-------------------------------------------------


KAMPUNI 19 zinazomilkiwa na wazawa, jana Machi 11, 2024 zilihitimu mafunzo ya biashara yaliyowezeshwa na Mgodi wa Barrick North Mara ili ziweze kufanya biashara ndani na nje ya mgodi huo kwa ufanisi zaidi.

Wamiliki wa kampuni hizo ni wafanyabishara wanaotoka maeneo yaliyo jirani na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara.

“Kuhitimu kwa kampuni hizi ni alama muhimu katika kukuza biashara ya wazawa katika mkoa wetu wa Mara,” Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko alisema wakati wa mahafali ya kuhitimu kwa kampuni hizo yaliyofanyika mgodini hapo.


Mwakilishi wa Kampuni ya Kemanyanki akizungumza wakati wa mahafali hayo.
--------------------------------------
GM Lyambiko alisema Kampuni ya Barrick Gold imeendelea kuwapa wazabuni wazawa fursa za kuhudumia na kusambaza bidhaa katika mgodi huo ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo hayo.

Alitolea mfano wa Dola za Marekani milioni 37.4 sawa na takriban shilingi bilioni 95 ambazo zimelipwa na mgodi huo kwa wazabuni wazawa kwa mwaka 2023 huku ukitilia maanani falsafa ya ‘Local Content’.

Meneja Mkuu huo alisema hadi sasa mgodi wa Barrick North Mara umesajili kampuni 118 ambazo zinapata fursa mbalimbali za kibiashara katika mgodi huo.

Jambo la kufarahisha ni kwamba kampuni hizo za wazawa zimetoa ajira kwa watu 1,144, wengi wao wakiwa ni ambao wanatoka katika maeneo yanayozunguka mgodi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.


Mwakilishi wa Kampuni ya Timbo akipokea kutoka kwa DC Chikoka cheti cha kuhitimu mafunzo hayo. Wa pili kushoto ni Meneja Mkuu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko.
---------------------------------------
“Jitihada hizi sio tu zimechangia kweye ustawi wa maendeleo ya jamii bali zimesaidia katika kuimarisha mahusiano yetu na jamii inayotuzunguka,” alisema GM Lyambiko.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara katika mahafali hayo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Rorya, Juma Chikoka aliipongeza Kampuni ya Barrick Gold kwa kuanzisha mpango wa kuendeleza wafanyabiashara wazawa katika mgodi wa North Mara.

DC Chikoka alisema mpango huo una faida nyingi ikiwemo kusaidia kuongeza mapato ya Serikali, kutengeneza ajira kwa vijana na kukuza uchumi.

“Kama Serikali tunatambua mchango wa Barrick North Mara, na hii inatusaidia pia kufikia maendeleo ya kitaifa,” alisema Chikoka ambaye pia kwa sasa ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tarime.


DC Chikoka akizungumza 
wakati wa mahafali hayo.
--------------------------------------
Mwakilishi kutoka Tume ya Madini, Annasia Kwayu naye pia aliupongeza mgodi huo kwa kufanikisha mafunzo hayo ambayo yameendeshwa na Kampuni ya Impacten na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia huduma bora katika mgodi nchini.

“Tunawapongeza wahitimu na Kampuni ya Barrick. Tunatarajia wazabuni watatoa huduma bora za kimataifa,” alisema Kwayu ambaye ni Meneja Ukaguzi wa Fedha, Kodi na Ushirikishwaji wa Watanzania kutoka Tume ya Madini.


Annasia Kwayu akizungumza 
wakati wa mahafali hayo.
----------------------------------------
Kwayu alisema mpango huo ni kielelezo halisi cha utekelezaji wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na kanuni za ushirikishwaji wa Watanzania za Mwaka 2018 na marekebisho yake.

Mhamasishaji maarufu (motivational speaker) nchini, Joel Nanauka alipata fursa ya kuzungumza na wahitumu hao kwa dakika kadhaa na kuwataka kuwa na maono ziadi huku wakijiepusha na watu wasiokuwa na maono.

Nanauka alielezea mpango wa mafunzo hayo kwa wafanyabiashara wazawa kama jambo muhimu na uwekezaji mkubwa.


Mhamasishaji Nanauka akiwa kazini 
wakati wa mahafali hayo.
--------------------------------------
Nao wahitimu wa mafunzo hayo ambayo yamechukua miezi sita waliishukuru Kampuni ya Barrick huku wakiahidi kufanya vizuri zaidi katika biashara zao.

“Sio tu kwamba tumejengwa uwezo wa kufanya biashara zetu vizuri na kwa ufanisi na mgodi wa Barrick, bali pia katika kufikiri nje ya ‘box’ kutafuta kazi nje ya mgodi wa Barrick,” alisema mmoja wa wahitimu hao.

Aidha, wahitimu hao waliahidi kuwa walipaji wazuri wa kodi za Serikali sambamba na kuwa mabalozi wazuri wa wazabuni wanaofanya biashara na mgodi huo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages