NEWS

Tuesday 12 March 2024

Waziri Mkuu wa Haiti aripotiwa kujiuzuluAriel Henry
--------------------------

WAZIRI Mkuu wa Haiti, Ariel Henry amejiuzulu, Mwenyekiti wa kundi la nchi za Caribbean amesema, kufuatia wiki za shinikizo na kuongezeka kwa ghasia nchini humo.


Inakuja baada ya viongozi wa kanda kukutana nchini Jamaica jana Jumatatu kujadili mpito wa kisiasa nchini Haiti.

Kwa sasa Henry yuko Puerto Rico baada ya kuzuiwa na magenge yenye silaha kurudi nyumbani. Alikuwa ameiongoza nchi hiyo tangu kuuawa kwa Rais Julai 2021.

Akizungumza kufuatia mkutano huo mjini Kingston, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Caribbean na Rais wa Guyana, Irfaan Ali alisema: "Tunatambua kujiuzulu kwake baada ya kuanzishwa kwa baraza la mpito la rais na kumtaja waziri mkuu wa muda."

Magenge yenye silaha kali yamedhibiti mitaa ya mji mkuu wa Haiti wa Port-au-Prince katika siku za hivi karibuni, yakitaka Waziri Mkuu huyo ambaye hajachaguliwa ajiuzulu.

Henry alikuwa nchini Kenya kutia saini mkataba wa kutumwa kwa kikosi cha usalama cha kimataifa kusaidia kukabiliana na ghasia wakati muungano wa magenge uliposhambulia vituo vya polisi na kuvamia magereza mawili makubwa zaidi nchini Haiti.

Ndege iliyokuwa imembeba Henry ilizuiwa kutua kufuatia msururu wa mashambulizi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Haiti.

Ameelezea nia ya kurejea Haiti lakini hali ya usalama inahitaji kuimarishwa kabla hajaweza kufanya hivyo, kulingana na Marekani iliyokuwa kwenye mazungumzo mjini Kingston jana Jumatatu.

Afisa Mkuu wa Marekani alisema Henry alifikia uamuzi wa kujiuzulu Ijumaa iliyopita lakini alikuwa akisubiri tangazo rasmi ili mazungumzo yafanyike.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Blinken alitoa Dola milioni 100 kwa ajili ya kikosi cha usalama kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa chenye askari 1,000 ambacho Kenya inatarajiwa kuongoza nchini Haiti.

Mchango uliopendekezwa wa Marekani kwa kikosi cha usalama sasa unafikia Dola milioni 300 kufuatia tangazo la Blinken, na Dola milioni 33 zaidi zimetengwa kwa ajili ya misaada ya kibinadamu.

Kundi la Caricom la viongozi wa Caribbean, pamoja na Marekani na wawakilishi kutoka Haiti, pia walijadili mfumo wa mpito wa kisiasa.

Rais Ali alisema Baraza la Mpito la Rais litakuwa na waangalizi wawili na wajumbe saba wanaopiga kura, wakiwemo wawakilishi kutoka miungano kadhaa, sekta ya kibinafsi, mashirika ya kiraia na kiongozi mmoja wa kidini.

Baraza limepewa mamlaka ya "haraka" kumteua waziri mkuu wa muda, alisema na kuongeza kuwa yeyote anayenuia kugombea katika uchaguzi ujao wa Haiti hataweza kushiriki.

Baraza hilo linatarajiwa kuongoza Haiti kuelekea kwenye uchaguzi wa kwanza tangu mwaka 2016.

Henry, aliyekuwa mamlakani tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moïse, alikuwa ameahirisha uchaguzi mara kadhaa, akisema usalama lazima urejeshwe kwanza.

Ya msingi kuhusu Haiti:
Nchi hii inashirikishana mpaka na Jamhuri ya Dominika na inakadiriwa kuwa na wakazi milioni 11.5.

Ina eneo la ardhi la kilomita za mraba 27,800, ambalo ni dogo kidogo kuliko Ubelgiji na karibu ukubwa sawa na jimbo la Maryland la Marekani.

Ukosefu wa utulivu wa miaka mingi, udikteta na majanga ya asili katika miongo ya hivi karibuni yameiacha Haiti kuwa taifa maskini zaidi katika bara la Amerika Kaskazini.

Tetemeko la ardhi mwaka 2010 liliua zaidi ya watu 200,000 na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu na uchumi.

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kiliwekwa mwaka 2004 kusaidia kuleta utulivu nchini humo na kiliondoka mwaka 2017.

Julai 2021, Rais Jovenel Moïse aliuawa na watu wenye silaha wasiojulikana huko Port-au-Prince. Huku kukiwa na mkwamo wa kisiasa, nchi hiyo inaendelea kukumbwa na machafuko na ghasia za magenge.
Chanzo: BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages