NEWS

Thursday 14 March 2024

Katibu Mkuu UWT CCM azuru Tarime, aweka jiwe la msingi jengo la makazi ya mtumishiKatibu Mkuu wa UWT CCM, Jokate Mwegelo akipiga makofi mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika jengo la makazi ya mtumishi wa Umoja huo lililopo kata ya Nyandoto, Halmashauri ya Mji wa Tarime jana.
----------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Tarime
-------------------------------------


KATIBU Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jokate Mwegelo, jana alikagua na kuweka jiwe la msingi katika jengo la makazi ya mtumishi wa Umoja huo, lililopo kata ya Nyandoto katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.

Pia Jokate alikabidhi kadi kwa wanachama wapya wa kike 100 waliojiunga na UWT, na kuagiza Umoja huo kuendelea kusajili wanachama zaidi.

Katibu Mkuu wa UWT, Jokate na viongozi wengine wa Umoja huo ngazi ya mkoa na wilaya wakiwa katika picha ya pamoja na wanachama wapya.
------------------------------------------

Jokate ambaye alikuwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya UWT wilayani Tarime, aliipongeza UWT Wilaya ya Tarime kwa kutelekeza maagizo ya kujenga nyumba za watumishi wa Umoja huo, na kuchangia fedha taslimu shilingi milioni tano.


Jokate alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wanawake nchini kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.

Aidha, aliwataka wananchama wa UWT kushiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi na kuhakikisha wagombewa wa CCM wanashinda uongozi wa vijiji, mitaa na kata kwa kishindo.

“Wanawake jitokezeni kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, wanawake ndio wapigakura wanaotegemewa na CCM, tuwe wapigakura lakini pia tugombee," alisema Katibu Mkuu huyo wa UWT.Awali, Mwenyekit wa UWT Wilaya ya Tarime, Neema Charles alimpongeza Katibu Mkuu Jokate kukubali kuja Tarime na kuwawekea jiwe la msingi katika jengo la mtumishi wa Umoja huo.

“Tunakupongeza sana kuja Tarime, nadhani umeona kitu hapa [jengo], naomba useme kitu ili nyumba hii ikamilike,” alisema Neema.


Katika hatua nyingine, uongozi wa UWT Mkoa wa Mara umemkabidhi Jokate tuzo maalumu kutokana na kazi nzuri anazozifanya kwa uhodari, uadilifu, ubunifu na uzalendo wa kweli.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages