NEWS

Wednesday 13 March 2024

Rais Samia ashangazwa wananchi kukosa kituo cha afya licha ya mgodi wa North Mara kumimina mabilioni ya fedha Tarime Vijijini



Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza leo Ikulu jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni.
--------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu
---------------------------------

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ameendelea kutilia mkazo suala la matumizi mazuri ya fedha zinazotolewa na wawekezaji, wakiwemo wa uchimbaji dhahabu, kupitia mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

Kiongozi huyo wa nchi amesisitiza suala hilo Ikulu jijini Dar es Salaam leo, mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni, wakiwemo Wakuu wa Mikoa.

Ametoa mfano wa taarifa za kushangaza ambazo amewahi kuziona kwenye moja ya chombo cha habari hapa nchini, zikionesha wananchi wakilalamika kukosa kituo cha afya licha ya kuishi karibu na Mgodi maarufu wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

Rais amekiri kufahamu kwamba mgodi huo unatoa fedha nyingi kwa ajili ya kugharimia miradi ya kijamii katika maeneo yanayouzunguka kupitia mpango wake wa CSR.

“Najua North Mara wanatoa pesa, mnaotoka huko mlianglie hili,” Rais Samia ameagiza.

Mgodi wa North Mara umekuwa mstari wa mbele kwa kutoa mamilioni ya fedha kwa ajili ya kugharimia miradi mbalimbali ya kijamii kama vile elimu, afya, maji na barabara, ikiwa ni sehemu ya wajibu wake kwa wananchi wenyeji.

Hivi karibuni, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) ilipitisha mpango wa matumizi ya shilingi bilioni tisa za CSR kutoka Barrick North Mara.

Kiasi hicho cha fedha ni mbali na shilingi zaidi ya bilioni saba zilizotolewa na mgodi huo na tayari zimetumika kugharimia utekelezaji wa miradi ya kijamii katika miezi ya hivi karibuni.

Mbali na kupata fedha za CSR, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini pia inapata mabilioni ya fedha za Ushuru wa Huduma (Service Levy) kutoka mgodi huo ambao unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Rais Samia ametumia fursa ya uapisho wa wateule wake kutoa onyo dhidi ya kuzuka kwa vikundi hewa vinavyotumika kukwapua fedha za Serikali katika ngazi ya halmashauri.

“Vikundi bandia vinaundwa, fedha zinalipwa na ile ni fedha ya Serikali ambayo imekusudiwa kwa maendeleo ya wananchi na siyo tu kuliwa na madiwani,” ameonya Rais Samia.

Akizungumzia uongozi usiokuwa na dosari, Rais amewataka Wakuu wa Mikoa kujitambua na kudumisha uhusiono mzuri katika maeneo yao ya kazi, huku akisema baadhi ya viongozi hao wanafanya mambo ya ajabu - ambayo hata hivyo hakuyataja.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages