NEWS

Monday 18 March 2024

Miaka mitatu ya Rais Samia: TANROADS Mara yatekeleza miradi mikubwa iliyogharimu mabilioni ya fedha, Mhandisi Maribe amshukuru Rais na wasaidizi wake



Sehemu ya barabara ya Nyamuswa - Bunda - Bulamba (kilomita 56.4) iliyotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 67.887 chini ya usimamizi wa TANROADS Mkoa wa Mara.
-----------------------------------------------


NA MWANDISHI MAALUMU

----------------------------------------------


WAKALA ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara imetangaza mafanikio iliyopata katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamburi ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Mafanikio hayo yamejikita katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara, madaraja, Uwanja wa Ndege Musoma, mizani ya kupima uzito wa magari na uwekaji wa taa na alama za barabarani.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari wilayani Bunda wiki iliyopita, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe alianza kwa kubainisha mtandao wa barabara zinazohudumiwa na ofisi yake.

Alisema kuna barabara kuu zenye urefu wa kilomita 409.73 zikiwemo za lami (km 219.67) na changarawe (km 190.06), barabara za mkoa zenye urefu wa kilomita 1,017.19 (lami km 170.52 na changarawe (km 846.67) na madaraja 495 yenye ukubwa tofauti.

Mhandisi Maribe aliweka wazi kuwa katika kipindi hicho cha miaka mitatu ya Rais Samia, Serikali Kuu imeweza kuutengea mkoa wa Mara shilingi bilioni 59.378 kwa ajili ya kugharimia matengenezo ya barabara na madaraja.

Miradi iliyokamilika
Meneja huyo wa TANROADS Mara alitaja miradi mikubwa iliyotekelezwa na kukamilika katika kipindi hicho kuwa ni ujenzi wa barabara tatu kwa kiwango cha lami - zenye urefu wa kilomita 111.4 kwa gharama ya shilingi bilioni 137.165.

Barabara hizo ni Nyamuswa - Bunda - Bulamba (km 56.4) iliyotekelezwa na mkandarasi CCECC kwa gharama ya shilingi bilioni 67.887 na ile ya Makutano Juu - Sanzate (km 50) iliyojengwa na Mbutu Bridge JV kwa shilingi bilioni 60.99.

Nyingine ni Kusenyi - Suguti (km 5) iliyotekelezwa na Kampuni ya Gemen Engineering Ltd kwa shilingi bilioni 8.288 ambayo ni sehemu ya barabara ya Musoma - Busekela yenye urefu wa kilomita 92.

Aidha, Serikali ilitoa shilingi bilioni 4.4 ambazo tayari zimetumika kugharimia shughuli za kuifungua barabara ya kuingia Hifadhi ya Taifa Serengeti iliyokuwa haipitiki kirahisi. Barabara hiyo ni Tabora B - Klens Gate yenye urefu wa kilomita 54, inayounganisha mkoa wa Mara na Arusha.

Taa za barabarani
Kwa upande mwingine, Mhandisi Maribe alisema ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia, Serikali kupitia TANROADS Mkoa wa Mara imefanikiwa kuweka taa za sola za barabarani zenye thamani ya shilingi bilioni 2.8.

“Taa hizo zimewekwa katika maeneo mbalimbali mkoani Mara, ikiwemo mjini Musoma, Bweri, Nyabange, Butiama, Kiabakari, Pida, Isabasaba, Makutano (Ziroziro), Mazami, Nyanchabakenye, Utegi, Mika, Buhemba, mjini Tarime na Sirari.

“Aidha, katika mwaka huu wa fedha tutaweka taa 336 katika maeneo ya Kusenyi, Musoma Manispaa, Nyamuswa, Bitaraguru, Nyamika na Olio. Pia katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita tumeweza kuweka alama za barabarani katika maeneo mbalimbali mkoani,” alisema Mhandisi Maribe.


Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe akizungumza na waandishi wa habari.
----------------------------------------------

Miradi inayoendelea
Kwa upande mwingine, Meneja Maribe alisema Serikali Kuu ilitenga shilingi bilioni 212.576 ambazo zitatumika kugharimia miradi mitano inayoendelea kutekelezwa chini ya usimamizi wa TANROADS katika maeneo mbalimbali mkoani Mara.

Alitaja mradi wa kwanza kuwa ni ujenzi wa barabara ya Sanzate - Natta (km 40) inayounganisha wilaya ya Bunda na Serengeti kwa kiwango cha lami, ambayo inatekelezwa na kampuni ya CRSG Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 39.469.

Mradi wa pili unaoendelea kutekelezwa alisema ni ujenzi wa barabara ya Mogabiri - Nyamongo (km 25) kwa kiwango cha lami, unaojengwa na mkandarasi Nyanza Road Works kwa shilingi bilioni 34.662.

Meneja Maribe alitaja mradi wa tatu kuwa ni barabara ya Tarime - Mugumu (km 87.14), sehemu za Tarime - Mogabiri (km 9.3), Nyamongo - Mugumu (km 48.15) na barabara ya mzunguko ya Mugumu (km 3.6) unaotekelezwa na STECOL kwa shilingi bilioni 81.149.

Mradi wa nne, alisema ni ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma (km 1.705) unaotekelezwa na BCEG Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 35.048, na mradi wa tano ni ujenzi wa mzani wa kupima uzito wa magari yakiwa kwenye mwendo wilayani Bunda, unaotekelezwa na CHICO Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 22.248.

Miradi inayosanifiwa
Katika hatua nyingine, Meneja Maribe alitaja miradi mitatu inayofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika maeneo tofauti mkoani Mara.

Miradi hiyo ni barabara ya Nyankanga - Rung’abure (km 91) inayounganisha wilaya za Butiama na Serengeti, chini ya Mhandisi Mshauri aitwaye Edge Consulting Ltd kwa gharama ya shilingi milioni 410.5, Kuruya - Kinesi (km 18.42) wilayani Rorya, chini ya Mhandisi Mshauri aitwaye UWP Consulting kwa shilingi milioni 184.9 na Balili - Mugeta Chini (km 41.43) wilayani Bunda.

Aidha, Meneja huyo wa TANROADS alitaja miradi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami inayotarajiwa kutekelezwa mkoani Mara kuwa ni Musoma - Kusenyi (km 40) katika barabara ya Musoma - Busekela wilayani Musoma, na Mika - Utegi - Shirati - Kirongwe (km 56.8) wilayani Rorya.

Kwa mujibu wa Mhandisi Maribe, miradi mingi imefanikishwa na wakandarasi wazawa, ikiwa ni juhudi za makusudi zinazofanywa na Serikali ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa ya matengenezo ya barabara.

Alitaja miradi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami iliyotekelezwa na wakandarasi wazawa kuwa ni Makutano - Sanzate (km 50) uliojengwa na Mbutu Bridge JV, Kusenyi - Suguti (km 5) uliotekelezwa na Gemen Engineering na Mogabiti - Nyamongo (km 25) unaojengwa na Nyanza Road Works. Aidha, miradi yote ya matengenezo ya Barabara na madaraja ilitekelezwa kwa kutumia wakandarasi Wazawa.

“Mvua za el-nino zilizoanza mwaka jana hazijaleta madhara makubwa katika barabara za mkoa wa Mara. Maeneo yote yaliyopata matatizo yalishughulikiwa kwa haraka, hivyo hakuna barabara iliyokatika na kujifunga kutokana na mvua hizo,” alisema Mhandisi Maribe.

Faida za miradi hiyo
Utekelezaji wa miradi mbalimbali chini ya TANROADS mkoani Mara katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia, umekuwa na faida nyingi, mojawapo ikiwa ni ajira kwa watu 641, wakiwemo Watanzania 601 sawa na asilimia 93.7 ya waajiriwa wote.

Mhandisi Maribe alitaja faida nyingine za kiuchumi kuwa ni kuwaongezea wananchi kipato kutokana na ajira na biashara za kuuza bidhaa kwa wafanyakazi, zikiwemo huduma za vyakula kutoka kwa mama na baba lishe.

Pia kurahisisha usafiri na ushafirishaji, kuchochea ukuaji wa biashara ya dhahabu kwa kuwa barabara nyingi zinapita maeneo ya uchimbaji wa madini hayo, lakini pia kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo na mifugo na usafiri wa watalii kwenda na kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Meneja huyo wa TANROADS alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanakuwa walinzi wa miundombinu ya barabara zikiwemo taa na alama za barabarani, huku akitahadharisha kuwa mtu yeyote atakayebainika kuiba na kuharibu miundombinu ya barabara atakamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu Uchumi.

“Pia ninaomba wananchi waheshimu maeneo ya hifadhi za barabara kwani kufanya shughuli kwenye eneo la hifadhi ya barabara ni kosa. Na kwa upande wa madereva waepuke kuzidisha uzito kwenye magari na kumwaga mafuta na oil barabarani ili kuzilinda ziweze kudumu muda mrefu kwa manufaa ya jamii nzima,” alisisitiza.

Amshukuru Rais Samia
Meneja Maribe alihitimisha kwa kumshukuru Rais Samia kwa kuidhinisha fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara na miundombinu yake mkoani Mara.


Rais Samia Suluhu Hassan
----------------------------------------

Aliwashukuru pia Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na wasaidizi wake, pamoja na Mtendaji Mkuu wa TANROADS kwa kuendelea kumpa mwongozo wa kujenga barabara bora na kuhakikisha ofisi yake haikwami kutekeleza majukumu yake.

Mhandisi Maribe pia aliwashukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa mkoa huo, Patrick Chandi Marwa, wabunge na wafanyakazi wenzake wa TANROADS kwa jinsi wanavyoendelea kumpa ushirikiano wa dhati katika utekelezaji wa majukumu ya kiofisi.

Waziri Mkuu ampongeza
Akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mara Hivi karibuni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimpongeza Mhandisi Maribe kwa uwezo wake wa uthubutu na ubunifu katika ujenzi wa barabara za lami mkoani humo.

“Asante sana Injinia (Mhandisi), nimefurahi kusikia kwamba TANROADS hapa mkoani wamejiongeza kwa kuona umuhimu wa barabara ya Kuruya mpaka Kinesi Bandarini, huko ni kujiongeza - mpigieni makofi Meneja wa TANROADS.

“Kwa hiyo Meneja wa TANROADS [Mhandisi Maribe] hongera kwa kuiona hii barabara kwamba ina umuhimu wake, inaenda bandarini eneo la uvuvi, hongera sana Meneja wa TANROADS mnaendelea vizuri,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa na kuitaka Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kuiunga mkono ofisi ya Meneja huyo katika jitihada za ujenzi wa barabara hiyo.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages