NEWS

Monday 25 March 2024

Mkurugenzi wa Haki za Binadamu Tarime aupa tano mgodi wa Barrick North Mara kwa kuzingatia haki za binadamu



Mkurugenzi wa Shirika la Tuwakomboe Paralegal, Bonny Matto.
----------------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU
-----------------------------------------


SHIRIKA la sheria na haki za binadamu la Tuwakomboe Paralegal (TPO) lililopo wilayani Tarime, limesema kwa sasa kuna mabadiliko makubwa kuhusu uzingatiaji wa haki za binadamu katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara ukilinganisha na miaka ya nyuma.

“Kwa miaka hii miwili - mitatu, nasema kutoka sakafu ya moyo wangu, Barrick North Mara Mine wanazingatia haki za binadamu, wanafanya mambo tofauti na miaka ya nyuma,” alisema Mkurugenzi wa shirika hilo, Bonny Matto katika mahojiano maalum na Sauti ya Mara mjini Tarime wili iliyopita.

Kutokana hali hiyo, Matto alisema malalamiko kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu kutoka kwa jamii inayozunguka mgodi huo yamepungua.

“Miaka ya nyuma watu walikuwa na malalamiko mengi dhidi ya mgodi lakini sasa hivi yamepungua sana, hakuna malalamiko kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu, haki za binadamu zimezingatiwa kwa kiwango kikubwa,” alisisitiza na kufafanua zaidi:

“Kuna vitu vingi vinavyothibitisha hali hiyo, mfano walinzi wote wa mgodi wa Barrick North Mara hawabebi silaha, na hakuna mwananchi anayelalamika kwamba amepigwa na mlinzi wa mgodi, hayo ni maendeleo makubwa ukilinganisha na ilivyokuwa zamani.”

Matto alitaja mambo mengine yanayodhihirisha uzingatiaji wa haki za binadamu katika mgodi huo kuwa ni pamoja na uboreshaji wa huduma za kijamii kutokana na fedha zinazotolewa na Barrick North Mara kupitia mpango wake wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

Alifafanua kuwa huwezi kuzungumzia haki za binadamu bila kuijali jamii inayokuzunguka kwa kuhakikisha inapata huduma bora za kijamii.

“Ukishughulikia mambo ya haki za binadamu lazima utazame pia huduma za kijamii kama maji. Tunaona mgodi wa Barrick North Mara umesambaza maji ya bomba kwa wakazi wa vijiji vinavyopakana nao, umejenga tenki kubwa la maji kule Nyamongo wananchi wanapata maji.

“Kitu kingine ni elimu, mgodi umesaidia kujenga miundombinu ya shule katika vijiji vilivyo jirani - shule zimeboreshwa, hapo pia wamezingatia haki ya binadamu ya kupata elimu. Haya yote ni mambo ya msingi sana, mimi ninaupongeza mgodi huo kwa kazi kubwa unayoifanya kwa ajili ya wananchi wa Tarime,” alisema Matto.

Alizungumzia pia suala la mazingira akisema mgodi wa Barrick North Mara umeonesha mananikio makubwa katika kuhakikisha uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji hautokei kutokana na shughuli zake za utafiti na uchimbaji madini.

“Tukiangalia miaka ya nyuma, kulikuwa na uchafuzi wa mazingira na maji ya mto Tigithe ulio jirani na mgodi huo, lakini sasa hivi hakuna tatizo hilo, wametengeneza miundombinu inayokusanya majitaka na kuyatibu kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

“Siku hizi hakuna mtu anayelalamika kwamba ng’ombe wake wamekufa kwa kunywa maji ya mto Tigithe, mgodi umedhibiti kila kitu - mambo yanaenda vizuri,” alisema Matto.

Alisisitiza kuwa mgodi wa Barrick North Mara unapastahili kupongezwa kutokana na mageuzi makubwa unayofanya katika jitihada za kuwaletea wananchi maeneleo ya kijamii na kiuchumi.

“Lazima tu- appreciate (tuthamini) shughuli zinazofanywa na mgodi, wananchi wawe na mtazamo chanya kuhusu mgodi wa Barrick North Mara, ile mitizamo hasi juu ya mgodi huo iondoke,” alisema.

Matto alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba wananchi kusaidia kulinda mgodi huo dhidi ya vitendo vya uvamizi, wizi wa mawe ya dhahabu na uharibibu wa miundombinu yake ili uendelee kuzalisha na kunufaisha jamii.

“Wananchi tukiwa walinzi wa kuangalia watu wasiingie kuvamia mgodi, kuiba mali na kuharibu miundombinu ya mgodi, uchumi wa Nyamongo na jamii kwa ujumla utainuka, zile hela wanazotumia kujenga fence (uzio) zingetumika kufanya maendeleo kwa wananchi wa Tarime.

“Tukemee na kalaani vitendo vya kuvamia mgodi huo ili uweze kufanya kazi kubwa na wananchi waweze kunufaika zaidi, tusiurudishe nyuma mgodi, tuusaidie kiulinzi kwa sababu una mchango mkubwa wa maendeleo kwa wananchi wa Tarime,” alisema Matto.

Hata hivyo, Matto Mkurugenzi huyo wa Shirika la Tuwakombe Paralegal alitoa wito kwa wananchi kutumia dawati la mahusiano katika mgodi huo kupata ufumbuzi pale wanapokuwa na malalamiko. “Kama kuna malalamiko watumie lile dawati la mahusiano, ni dawati ambalo limeboreshwa sana,” alisisitiza.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages