NEWS

Wednesday, 28 January 2026

TISEZA yaendesha semina kwa wadau ikizindua Dawati la Uwekezaji Mara




Na Mwandishi Wetu
Musoma
---------------

Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imefanya semina na wadau wa uwekezaji mkoani Mara kwa ajili ya kuhamasisha uwekezaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi zilizopo hapa nchini.

TISEZA iliendesha semina hiyo mjini Musoma, sambamba na kuzindua Dawati la Uwekezaji Mkoa wa Mara, Januari 26, 2026.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Dawati hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya TISEZA, Balozi Dkt. Aziz Mlima, alisema mamlaka hiyo inalenga kuwawezesha Watanzania kutumia fursa za uwekezaji kwa kuwapa unafuu wa mitaji kutokana na punguzo la kodi na ushuru wa forodha.

“Lengo la serikali ni kuongeza idadi ya wawekezaji ili kutekeleza Dira ya 2050 ambayo inalenga kukuza uchumi wa Tanzania kufikia Dola za Kimarekani zaidi ya trilioni moja kwa kuongeza wawekezaji wa ndani,” alisema Dkt. Mlima.

Aliongeza kwamba serikali imechukua hatua za makusudi kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuwahamasisha Watanzania zaidi kushiriki katika uwekezaji kwa kuwapa misamaha ya kodi na punguzo la ushuru wa forodha kwa baadhi ya bidhaa zinazotumika kwenye miradi ya uwekezaji, jambo linalolenga kuchochea wawekezaji zaidi.

Mwenyekiti huyo wa Bodi ya TISEZA pia alimpongeza Mwekezaji wa Mkoa wa Mara, Emille Gotham, kwa kuanzisha mchakato wa kuwekeza katika uzalishaji wa chakula cha samaki na kumhakikishia soko la uhakika kutokana na serikali kuwahamasisha wananchi kufuga samaki katika vizimba na kwamba kwa sasa chakula hicho kinatoka nje ya Tanzania.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Uhamasishaji Uwekezaji TISEZA, Geore Mukono, alisema kampeni hiyo itaonesha fursa mbalimbali zilizopo katika mikoa, taratibu za usajili wa miradi ya uwekezaji kwa lengo la kupata vyeti vya uwekezaji na leseni katika maeneo maalum ya kiuchumi, vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kwa wawekezaji hapa nchini.

Mukono alisema wawekezaji watakaojisajili watapata unafuu wa ushuru wa forodha hadi asilimia 100 na msamaha wa kodi hadi asilimia 75 katika vifaa vinavyotumika kwenye uwekezaji baada ya mradi husika kusajiliwa.

Alitolea mfano wawekezaji katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba wanaweza kupata msamaha wa kodi hadi asilimia 75 katika ununuzi wa boti, injini, ndoano, magari ya kusafirishia samaki, vizimba, neti na kadhalika.

Naye Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Gambaless Timotheo, aliishukuru TISEZA kwa kuhamasisha uwekezaji katika mkoa wa Mara na kuwataka wafanyabiashara na taasisi za kifedha kushirikiana kuanzisha miradi ya uwekezaji.

Gambales aliishukuru TISEZA pia kwa kuzindua Dawati la Uwekezaji Mkoa wa Mara na kuahidi kuwa mkoa huo utawasaidia Watanzania wanaotaka kuwekeza kupata taarifa na msaada watakaohitaji.

Mfanyabiashara Annastazia Omollo, mkazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, yeye aliiomba TISEZA kupeleka fursa za uwekezaji katika maeneo ya vijijini ili wananchi wengi zaidi waweze kuzisikia na kuzichangamkia.

“Wananchi wengi wa vijijini wanakosa fursa za kiuchumi kwa sababu ya kutofikiwa na programu mbalimbali za serikali na wadau,” alisema Omollo.

Alisema vijijini kuna wakulima na wafugaji wengi wenye mashamba makubwa na wanaomiliki idadi kubwa ya mifugo ambao wakipata elimu watafanya shughuli zao kisasa na kuwekeza zaidi na hatimaye kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na TISEZA na taasisi nyingine.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo Mkoa wa Mara, Denis Nyakisinda, alisema taasisi hiyo imeandaa mkutano wa wafanyabiashara na watendaji wa taasisi zote za serikali mkoani Mara utakaofanyika Februari 2026.

Aidha, Nyakisinda alisema kuwa taasisi hiyo inaandaa kongamano la wafanyabiashara wa mkoani Mara hivi karibuni na kuwataka wafanyabiashara kujiunga nayo na kushiriki matukio hayo ili kupata taarifa.

Semina hiyo ni sehemu ya Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani iliyoanza Januari 18 na itaendelea hadi Aprili 9, 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara, ambapo imeanza katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ikiwa na kaulimbiu inayosema ”Unawezeshwa Kuwekeza kwa Kupewa Unafuu wa Mtaji”.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages