NEWS

Saturday 9 March 2024

Rais Samia amteua Chongolo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, RAS Msalika ahamishiwa Rukwa, DC Mntenjele apelekwa TandahimbaRais Dkt Samia Suluhu Hassan
------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
----------------------------


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART).

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt Moses Kusiluka leo Machi 9, 2024, Rais Samia amefanya mabadiliko hayo kuboresha utendaji kazi wa Serikali yake.

Hivyo amemteua Daniel Godfrey Chongolo kuwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Songwe. Chongolo alijiuzulu nafasi ya Katibu Mkuu wa chama tawala - CCM miezi michache iliyopita.

Pia amewateua; Kanali Mstaafu Patrick Kenan Sawala aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba kuwa RC wa Mtwara na Paul Matiko Chacha kuwa RC wa Tabora.

Aidha, Rais Samia amewahamisha Wakuu wa Mikoa wanne, akiwemo Batilda Salha Burian kutoka Tabora kwenda Tanga.

Amewahamisha pia Makatibu Tawala wa Mikoa saba, wakiwemo Msalika Robert Makungu kutoka Mara kwenda Rukwa na Gerald Musabila Kusaya (Rukwa – Mara).

Wakati huo huo, kiongozi huyo wa nchi ameteua Wakuu wa Wilaya wapya watano, wakiwemo Festo Kiswaga kuwa DC wa Monduli na Kanali Evans Alfred Mtambi (DC wa Hanang’).

Amewahamisha Wakuu wa Wilaya 25, wakiwemo Kanali Michael Mangwela Mntenjele kutoka Tarime kwenda Tandahimba, Kanali Mauld Hassan Surumbu (Mkinga – Tarime), Joshua Samwel Nassari (Monduli – Magu), Kheri Denice James (Mbulu – Iringa) na Anna Joram Gidarya (Busega – Itilima).

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameteua Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri 10, wakiwemo George Stanlye Mbilinyi kuwa DED Bunda, Ummy Mohammed Wayayu (Ilemela) na Masud Salum Kibetu (Kahama).

Sambamba na uteuzi huo, amewahamisha Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri 25, wakiwemo Juma Haji Juma (Mbinga – Bunda Mji), Mohamed Ramadhan Ntandu (Nsimbo – Magu), Fidelica Gabriel Myovella (Magu – Mafinga Mji), Kibamba Kiomoni Kiburwa (Manispaa ya Ilemela – Jiji la Mwanza) na Aron Kagurumjuli (Jiji la Mwanza – Manispaa ya Ubungo).

Kwa upande mwingine, Rais Samia amemteua Waziri Waziri Kindamba aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa UDART, akichukua nafasi ya Gilliard Wilson Ngewe ambaye atapangiwa kazi nyingine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages