Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa (katikati), akiwa katika ziara fupi ya kutembelea Kituo cha Afya Magena, wilayani Tarime jana Jumapili, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya kimkoa ya Miaka 49 ya kuzaliwa kwa chama hicho.
Tarime
------------
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, amezindua maadhimisho ya kimkoa ya Miaka 49 ya kuzaliwa kwa chama hicho.
Uzinduzi huo ulifanyika siku ya Jumapili Februari 1, 2026 katika kata ya Nkende, wilayani Tarime, ambapo Chandi alikagua huduma za afya katika Kituo cha Afya Magena, na kuweka jiwe la msingi katika jengo la ofisi ya CCM ya kata hiyo.
"Tumekuja kikisemea CCM na Rais Samia Suluhu Hassan, ni mama wa kipekee sana, amefanya mambo makubwa na kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kwenye sekta za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara.
"Tumepita kwenye Kituo cha Afya kuangalia Ilani ya CCM kama inatekelezwa vizuri, hasa kwenye bima ya afya kwa wote ambayo Mama (Rais) aliinadi kwa wananchi na tumeona wanapata huduma bure.
"Niishukuru Kamati ya Siasa ya Tawi la Nkende kwa kubuni mradi wa ofisi, haya ndiyo mambo tunayotaka,” alisema Chandi.
Katika uzinduzi huo, Mwenyekiti Chandi aliambatana na viongozi mbalimbali wa ngazi ya mkoa na wilaya pamoja na wananchi.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment