NEWS

Friday 22 March 2024

Serikali kufuta maombi na leseni 2,648 za utafiti, uchimbaji madini



Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
---------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
-----------------------------------------


SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imemwelekeza Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kufuta maombi na leseni 2,648 za utafiti na uchimbaji wa madini ambazo wamiliki wake wamekuwa hawazingatii utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura 123.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, na kufafanua kuwa hatua hiyo inalenga kuwapa watu wengine fursa ya kuomba na kuendeleza maeneo ya leseni hizo kwa manufaa ya Taifa na ukuzaji wa sekta ya madini.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, miongoni mwa makosa ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara ni pamoja na wamiliki wengi wa leseni kutoanza, au kutoendeleza maeneo ya leseni zao, na badala yake kuhodhi maeneo, kutolipa ada stahiki za leseni, kutowasilisha nyaraka muhimu zikiwemo za Mpango wa Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Shughuli za Madini (Local Content Plan), Mpango wa Uwajibu wa Kampuni kwa Jamii (Corporate Social Responsibility - CSR) na taarifa za fedha kuonesha matumizi yaliyofanyika pamoja na vielelezo vya matumizi husika.

“Ninatoa mfano, kuna watu SITA tu wanahodhi maeneo yenye ukubwa wa ekari milioni 13, ukubwa wa maeneo hayo ni sawa na ukubwa mara nne wa Mkoa wa Kilimanjaro na hayafanyiwi chochote, ilihali mahitaji ya maeneo ya uchimbaji ni mkubwa sana hapa nchini, na hasa kwa wachimbaji wadogo ambao wamekuwa na mchango mkubwa sana kwenye kukuza sekta ya madini.

“Kuna watu wenye leseni za utafiti ambao hawatimizi masharti ya leseni zao, na hivyo kutegea uwepo wa wachimbaji wadogo kama mgongo wa utafiti wao," amesema Waziri Mavunde.

Kutokana na kosa la kutolipa ada stahiki za leseni, kiasi cha takriban shilingi bilioni 36 zinadaiwa kutoka kwa wamiliki na waliokuwa wamiliki wa leseni za utafutaji wa madini, uchimbaji mdogo wa madini, uchimbaji wa kati na mkubwa wa madini.

Kufuatia uwepo wa makosa hayo, Tume ya Madini imetoa Hati za Makosa kwa jumla ya leseni 59 hai kwa sababu wamiliki wake hawajatekeleza masharti na matakwa mbalimbali ya umiliki wa leseni husika.

Mbali na wamiliki wa leseni, kumekuwa na baadhi ya waombaji wa leseni ambao wamekuwa wakitumia vibaya fursa ya uwepo wa teknolojia rahisi ya uwasilishaji wa maombi ya leseni, yaani mfumo wa Online Mining Cadastre Portal, kwa kuwasilisha maombi mengi bila ya kulipa ada stahiki na wengine kuwasilisha maombi bila ya kuambatisha nyaraka zinazotakiwa kuwasilishwa pamoja na maombi ya leseni.

Katika uchambuzi uliofanywa na Tume ya Madini, imebainika kuwa hadi Februari 2024 kuna maombi 2,180 ambayo hayajalipiwa ada stahiki.

Vilevile, katika uchambuzi uliofanya na Tume ya Madini, imebainika kuwa hadi Februari 2024 kuna uwepo wa maombi 409 ya muda mrefu ambayo wamiliki wake wamelipa ada za maombi lakini hawajawasilisha nyaraka muhimu zinazoambatana na maombi hayo.

Mwelekeo wa serikali sasa ni kuona maeneo mengi yanagawiwa kwa vikundi vya wachimbaji wadogo na wawekezaji wenye uwezo wa kuchimba madini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages