NEWS

Thursday 7 March 2024

UWT CCM Tarime waadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kuonesha upendo kwa watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi MagufuliMwenyekiti wa UWT CCM Wilaya ya Tarime, Neema Charles akikabidhi msaada wa madaftari na kalamu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Magufuli mjini Tarime jana. Wa kwanza kushoto ni Katibu wa Jumuiya hiyo, Nyasatu Manumbu.
----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
--------------------------------------

JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime imeadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kuwatembelea wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Magufuli na kuwapatia msaada wa madaftari na kalamu, kisha kula nao chakula cha mchana.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo shuleni hapo jana, Mwenyekiti wa UWT Wilayani Tarime, Neema Charles alitoa wito kwa jamii kuwajali watoto wenye ulemavu kama watoto wengine kwa kuwapa elimu na haki nyingine za msingi.

“Wazazi na jamii tuwapende na kuwajali watoto wenye mahitaji maalum kwa kuwapa elimu kama watoto wengine. Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imejenga shule hii na inagharimia chakula kuhakikisha kila mtoto anapata elimu,” alisema Mwenyekiti huyo aliyefuatana na Katibu wake, Nyasatu Manumbu, miongoni mwa viongozi na wanachama wengine wa jumuiya hiyo.


Mwenyekiti Neema na wenzake wakipata chakula cha mchana pamoja na watoto hao.
--------------------------------------
Naye Mlezi wa UWT Wilaya ya Tarime, Noellah Gachuma alitoa wito wa kuihimiza jamii kuacha kasumba ya kuwafungia ndani watoto wenye ulemavu, badala yake wahakikishe wanawapa haki ya kupata elimu.

“Tusifungie watoto wenye mahitaji maalum ndani, kuwapeleka shule ni haki yao, unapomfungia ndani ni kumnyima haki yake,” alisema Noellah na kutumia nafasi hiyo pia kuwaomba wadau wa maendeleo kuungana katika kusaidia kundi hilo la jamii.


Noellah Gachuma
--------------------------
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Muguta Mununguli aliwashukuru wana-UWT hao kwa upendo wa kipekee waliouonesha kwa watoto.

“Nawashukuru sana UWT kwa kuja kuwaona hawa watoto, hii inawapa moyo wanafunzi hawa na kuona jamii inawajali, lakini pia ziara hii imewapa nafasi ya kujua changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye mahitaji maalum,” alisema Mwl Mununguli.

Shule ya Msingi Magufuli iliyopo mjini Tarime, ni ya wanafunzi wenye mahitaji maalum, ambapo kwa sasa wako 120 (wavulana 63 na wasichana 57) wa darasa la awali hadi la saba.

Kilele cha Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8 kila mwaka. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inasema “Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii.”

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages