NEWS

Thursday, 29 January 2026

Waziri Mkumbo: Tanzania Tuwekeze ni kampeni rasmi ya kitaifa



Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.

Na Mwandishi Wetu

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji imeitangaza Program ya Tanzania Tuwekeze kuwa kampeni rasmi ya kitaifa.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Januari 16, 2026 katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alitaja malengo ya kampeni hiyo kuwa ni kuelimisha umma kuhusu uwekezaji na kuhamasisha wananchi kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazotengenezwa na serikali.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Terri, alitangaza mpango wa utekelezaji unaohusisha mamlaka hiyo kuzunguka mikoa yote kuelimisha wawekezaji, wajasiriamali na wafanyabiashara kuhusu fursa za uwekezaji na vivutio vinavyotolewa na serikali kwa wawekezaji wa ndani.

Akizungumza na Gazeti la Sauti ya Marav wiki hii, Mbunifu wa Kampeni ya Tanzania Tuwekeze, Mkurugenzi Mkuu wa HAIPPA PLC, CPA Boniface Ndengo, aliipongeza Serikali na Wizara ya Mipango na Uwekezaji kurasimisha programu hiyo kuwa Kampeni ya Kitaifa.

CPA Ndengo alibainisha kwamba Juni 2025, HAIPPA PLC iliasisi Program ya Tanzania Tuwekeze ikiwa na malengo makuu ya kuelimisha umma kuhusu hisa na uwekezaji, kuhamasisha wajasiriamali na wabunifu wa Tanzania kujenga kampuni ili kutumia fursa za uwekezaji zinazotenegenezwa na serikali.

Alitaja malengo mengine kuwa ni kuhamasisha Watanzania wengi kushiriki katika fursa za uwekezaji kupitia hisa za kampuni za umma na kuwajengea uwezo wa kuwa na kipato cha pili kinachotokana na uwekezaji.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa HAIPPA PLC alisema alishaandikia Wizara ya Mipango na Uwekezaji, pamoja na TISEZA kuomba ushirikiano wa serikali kuhusu utekelezaji wa program hiyo.

CPA Ndengo ambaye pia ni Makamu Rais wa Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC), alikiri kuwa amepata barua kutoka Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji inayomhakikishia ushirikiano wa serikali na inayoelekeza TISEZA kushirikiana na HAIPPA PLC.

Alitaja makundi ya Wanufaika wa Kampeni ya Tanzania Tuwekeze kuwa ni pamoja na wajasiriamali, wabunifu wa miradi, wawekezaji wa ndani, watumishi, vijana na wananchi kwa ujumla.

Alibainisha kuwa kupitia kampeni hiyo, wabunifu, wajasiriamali na wafanyabiashara watapata ardhi, fursa za ubia, vivutio na mitaji inayopatikana kupitia nafuu za kikodi.


Mkurugenzi Mkuu wa HAIPPA PLC, CPA Boniface Ndengo,

Kwa upande wa watumishi na wananchi, CPA Ndengo alisema wanaweza kushiriki kwenye kampeni hiyo kwa kununua na kumiliki hisa za kampuni za umma kama HAIPPA PLC.

“Kimsingi tumefanya utafiti kwa kulinganisha nchi ambazo tulikuwa tunalingana kimaendeleo lakini leo wametuacha sana, mfano wake ni Korea Kusini,” alisema CPA Ndengo na kuendelea:

“Utafiti wetu umebaini kitu kinachoshtua akili kwamba nchini Korea Kusini elimu ya fedha na uwekezaji inafundishwa kuanzia shule za msingi na asilimia 44 ya wananchi wake wanamiliki hisa kwenye kampuni za uwekezaji zilizosajiliwa kwenye masoko ya hisa.”

CPA Ndengo aliongeza “Tanzania mbali na kuwa na makampuni machache ya Uwekezaji yasiyozidi 30 Wananchi wanaoshiriki kumiliki hisa za kampuni hizo ni pungufu ya asilimia moja. Takwimu hizo zinatupatia sababu ya HAIPPA PLC na serikali kuunganisha nguvu kufanikisha kampeni hii.”

Kuhusu faida, CPA Ndengo alisema kampeni hiyo ina faida nyingi kwa nchi na mwananchi mmoja mmoja, ikiwa ni pamoja na ufikiwaji haraka wa Dira ya Taifa ya 2050.

Alifafanua kuwa wananchi wengi watajumuishwa katika mfumo wa kifedha, bidhaa nyingi zitazalishwa ndani ya nchi, uwezo wa wananchi kuweka akiba na kuhudumia mahitaji ya familia utaongezeka, mabilionea wataongezeka na Pato la Taifa (GDP) kwa ujumla litaongezeka.

“HAIPPA tumejipanga kuhakikisha hatuachi mtu katika kampeni hii. Tumeweka mfumo rahisi wa usajili na elimu ambapo kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 anayemiliki simu ya mkononi anaweza kujisajili kwenye program.

“Tunayo pia mikakati mahususi ya kuwafikia watumishi, wakulima, wajasiriamali na vijana waliopo mtaani na vyuoni ili waunganishwe na kupatiwa elimu ya uwekezaji.

“Usajili unafanyika kupitia simu ya mkononi iwe kubwa au ndogo kwa kupiga namba ya huduma *149*46*23# au kutembelea Tovuti ya Haippa www.Haippa.Net au kupakua Application ya HAIPPA PLC Play store kisha omba kujisajili. Unaweza pia kupiga 0755 947 943 kupata msaada.

“Hii fursa ni kubwa sana kwetu Watanzania, tukiitumia vizuri Tanzania itaandika historia mpya kwenye dunia ya uwekezaji. Niwasihi Watanzania wote tujisajili ili tuunganishwe kwenye Program ya Tanzania Tuwekeze,” alisema CPA Ndengo.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages