NEWS

Wednesday 27 March 2024

Waziri Mkuu Majaliwa ataka uwekezaji ATCL uchochee ukuaji wa UchumiWaziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla ya mapokezi ya ndege mpya ya Shirika la Ndege Tanzania jijini Dar es Salaam jana Jumanne.
----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Dar
------------------------------------


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Uchukuzi kusimamia ipasavyo Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa unaleta matokeo chanya na kuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta nyingine mtambuka na uchumi kwa ujumla nchini.

Amesema kuwa ongezeko la ndege na huduma za usafiri linasaidia kuongeza fursa za biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine, kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na idadi ya watalii wanaokuja nchini.

Majaliwa aliyasema hayo wakati alipomwakilisha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 737-9 Max, kwenye uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam jana Jumanne.

Aidha, Waziri Mkuu alisema kuwa ili kuendelea kukuza sekta ya anga nchini, Wizara ya Uchukuzi iandae mpango wa kuongeza wataalamu wazalendo katika fani zinazohusu masuala ya ndege, hususan katika eneo la matengenezo na urubani.

Kadhalika, Majaliwa aliwataka watumishi wa ATCL kuongeza uzalendo na kuwafichua wote wenye nia ya kulihujumu shirika hilo pamoja na kudhibiti upotevu wa mapato kupitia tiketi na mizigo.

Pia aliwataka viongozi na watendaji wa shirika hilo kuhakikisha ndege zote zinaendeshwa kwa tija kwa kufanya tafiti za kutosha za masoko kabla ya kupeleka ndege.

Aliongeza kuwa usafiri wa anga umekuwa chachu ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na biashara. “Uwepo wa usafiri wa ndege umeongeza tija kubwa kwa wakulima, hususan wa mazao ya mbogamboga na matunda, wafugaji na wafanyabiashara wa Kitanzania,” alisema.

Katika Hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali ya Awamu ya Sita imesaini mikataba ya miradi mipya sita yenye thamani ya shilingi bilioni 674.3 inayohusu ujenzi wa kiwanda cha kujengea meli (shipyard) katika Ziwa Tanganyika, ujenzi wa meli kubwa ya kubeba mizigo tani 3,500 na meli nyingine yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mizigo ambayo inajengwa katika Ziwa Victoria.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa alisema sambamba na ununuaji wa ndege za abiria na moja ya mizigo, Serikali imenunua ndege mbili za mafunzo kwa ajili ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili kusaidia kuongeza idadi ya marubani kwenye soko la ajira na kupunguza uhaba wa marubani nchini.

“Pia NIT imewezesshwa mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya shahada na stashahada ya uhandisi wa ndege ili kuzalisha wahandisi na mafundi mchundo watakaoingia kwenye soko la ajira,” alisema Prof Makame.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi alimshukuru Rais Dkt Samia kwa kuendelea kuijengea kampuni hiyo uwezo wa kutoa huduma kwa kuinunulia ndege mpya na kuijengea miundombinu wezeshi katika biashara ya anga.

“Hadi sasa Serikali imewekeza shilingi trilioni 2.4 katika ununuzi wa ndege, ujenzi wa mindombinu wezeshi ya kibiashara pamoja na ulipaji wa sehemu ya madeni yaliyolimbikizwa,” alisema Mhandisi Matindi.

Aliongeza kuwa ATCL inaendelea kutekeleza mpango mkakati wake wa pili wa miaka mitano ulioanza mwaka wa fedha 2022/23 na kumalizia 2026/27 ambao pia unahusisha mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, yaani 2021/22-2025/26 ambao unatarajiwa kuiwezesha ATCL kuwa na ndege 20. “Hadi sasa ATCL ina ndege 14 zilizonunuliwa katika kipindi cha ufufuaji,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages