NEWS

Monday 25 March 2024

Waziri wa Madini afuta zuio la mgao wa mawe ya dhahabu mgodi wa Malera- NyamongoWaziri wa Madini, Anthony Mavunde.
-------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
---------------------------------------


WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde ametatua mgogoro baina ya wachimbaji wadogo wamiliki wa leseni na Kampuni ya KIRIBO katika mgodi wa Malera ambako kulikuwa na zuio la mgao wa mawe ya dhahabu.

Waziri Mavunde alitumia saa kadhaa kutatua mgogoro huo mgodini hapo jana Jumatatu, kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, watendaji wa wizara na viongozi wa wachimbaji wadogo mkoa huo (MAREMA).

“Ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan juu ya utatuzi wa migogoro mbalimbali katika sekta hii ya madini, ambayo inadhoofisha kukua kwa uzalishaji wa madini,” alisema Mavunde.

Waziri huyo mwenye dhamana ya madini alizipongeza pande zote kwa kuridhia makubaliano katika hatua ya awali ya kutatua mgogoro huo.

Alielekeza zuio la mgao wa mawe ya dhahabu yaliyozalishwa mgodini hapo liondolewe na mgao wa mawe uanze mapema leo Jumanne.

"Pia hakikisheni katika utekelezaji wa maridhiano haya, wachimbaji wadogo hawaondolewi katika eneo hilo na waachwe waendelee na shughuli zao,” aliagiza Waziri Mavunde.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda alimshukuru Waziri Mavunde kwa kufanikisha utatuzi wa mgogoro huo kwa kuruhusu mgao wa mawe uendelee kwani kipato cha wananchi wa eneo hilo kilikuwa kimeshuka na mapato ya serikali yalikuwa hayapatikani kwa wakati.

Watu zaidi ya 2,000 wananufaika na mgodi huo wa Malera uliopo wilayani Tarime, Mara ambao umekuwa ni shughuli kubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages