NEWS

Sunday 24 March 2024

USAID yafadhili ukarabati wa vyanzo 10 vya maji Mara kupitia WWFKatibu Tawala wa Wilaya ya Butiama, Rutagumirwa Rutalemwa (mwenye suti nyeusi) akikagua chanzo cha maji cha Kyanyamatende kilichoboreshwa na WWF Tanzania, kabla ya kukikabidhi kwa wakazi wa kijiji cha Buswahili wilayani Butiama jana Machi 23, 2024.
---------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Butiama
------------------------------------------


SHIRIKA la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) Tanzania limekabidhi chanzo cha maji cha asili Kyanyamatende kwa wakazi wa kijiji cha Buswahili wilayani Butiama, Mara.

Hicho ni miongoni mwa vyanzo vya maji vya asili vipatavyo 10 ambavyo shirika hilo limevifanyia maboresho na matunzo mkoani Mara, kupitia mradi wake wa Uhifadhi wa Dakio la Mto Mara, kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) Tanzania.

Makabidhiano ya chanzo cha maji cha Kyanyamatende yamefanyika sambamba na shughuli za usafi wa mazingira na upandaji wa miti kwa ajili ya kukihifadhi.


Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Butiama, Rutagumirwa Rutalemwa akipanda mti kando kando ya chanzo cha maji cha Kyanyamatende.
---------------------------------------------

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo jana Machi 23, 2023, Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Butiama, Rutagumirwa Rutalemwa alilishukuru Shirika la WWF kwa uboreshaji wa chanzo hicho cha maji na mazingira yanayokizunguka.

“Nawashukuru WWF chini ya ufadhili wa USAID, mmefanya jambo jema sana kukarabati na kuboresha chanzo hiki, na hii imepunguza adha ya maji,” alisema Rutagumirwa.

Alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuwahimiza wakazi wa kijiji cha Buswahili na wilaya ya Butiama kwa ujumla kutunza vyanzo vya maji na mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

“Jukumu la kutunza vyanzo vya maji ni endelevu katika maeneo yote tunayoishi. Tuepuke shughuli za mifugo, kilimo na ukataji miti kwenye vyanzo vya maji. Tukemee na kuwafichua watu wanaoharibu vyanzo vya maji. Ukimficha anayefanya hujuma nawe ni sehemu ya uharibifu wa chanzo hicho, tuendelee kutunza vyanzo vya maji kwa faida yetu na vizazi vijavyo,” alisema DAS huyo.


DAS Rutagumirwa akisoma hotuba wakati wa hafla hiyo.
-----------------------------------------

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Buswahili, Wambura Mwema aliyashukuru mashirika ya USAID na WWF kwa kuboresha chanzo hicho cha maji na kuahidi kusimamia utunzaji wake.

“Tumepata ukombozi, tutakitunza chanzo hiki cha maji, tutatunza miti 1,000 iliyopandwa na WWF katika eneo hili,” alisema Mwema na kubainisha kuwa chanzo hicho cha maji kinategemewa na kaya zaidi ya 800.

Nao wakazi wa kijiji cha Buswahili akiwemo Kadogo John Mwema, walisema uboreshaji wa chanzo cha maji Kyanyamatende umewaondolea adha waliyokuwa nayo ya kutumia maji machafu.

“Tunayo furaha sana hasa sisi akina mama kwa kuboreshewa chanzo hiki cha maji kwa sababu huko nyuma tulikuwa na shida sana, maji yalikuwa machafu sana, sasa hivi tumetengenezewa miundombinu ya maji na kujengewa uzio, tuko tayari kutunza chanzo hiki ili kidumu muda mrefu,” alisema Kadogo.


Makabidhiano ya mradi wa chanzo cha maji cha Kyanyamatende yakiendelea.
------------------------------------------

Awali, Afisa Ufatiliaji, Tathmini na Mafunzo kutoka WWF Tanzania, Enock Edward Rutaihwa alisema wanawezesha shughuli za utunzaji wa vyanzo vya maji kwa lengo la kuhifadhi dakio la mto Mara katika vijiji 125 vilivyoko kando kando ya mto huo kwenye wilaya sita za mkoa wa Mara.

“Mradi uliotukutanisha hapa unafadhiliwa na Watu wa Marekani, ndio waliofanya shughuli hii. Huu ni mradi wa miaka mitatu, ulianza mwaka Aprili 2022 na utafikia ukomo Aprili 2025,” alisema Rutaihwa.

Hafla hiyo pia ilihusisha maadhimisho ya Saa ya Dunia (Earth Hour) ambayo ni harakati ya kimataifa iliyoandaliwa na WWF, ambayo huhimiza watu binafsi, jumuiya na wafanyabiashara kupunguza matumizi ya nishati inayochangia uharibifu wa mazingira.

Jukumu kuu la Shirika la WWF wakati wa maadhimisho ya Saa ya Dunia ni kuunganisha watu kuchukua hatua kuhusu masuala ya kuhifadhi mazingira na kulinda sayari.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages